Na Mwandishi wetu
Mbunge wa Kigoma Kaskazini,Zitto
Kabwe, ameibuka mwanasiasa wa kwanza barani Afrika kutwaa tuzo ya mtetezi wa haki
ya hifadhi ya jamii, imefahamika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mwishoni mwa
wiki na Umoja wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya Nchi za Afrika Mashariki na Kati
(ECASSA), Zitto anatarajiwa kukabidhiwa tuzo yake hiyo katika sherehe rasmi
iliyopangwa kufanyika Oktoba 30 na 31 mwaka huu katika mji wa Livingstone
nchini Zambia.
“Tuzo hii imetolewa kwako kwa
kuzingatia mchango wako mkubwa unaoutoa kuhakikisha sehemu kubwa ya Watanzania
ambao walikuwa hawanufaiki na mifuko hii wanafaidika nayo,” ilisema taairifa
hiyo.
“ECASSA, mahususi kabisa,
imevutiwa na jitihada zako za kuhakikisha kwamba wasanii wananufaika na mifuko
ya hifadhi ya jamii pamoja na wakulima kupitia chama chao cha ushirika cha
Rumako kilichopo Kigoma Vijijini,” iliongeza sehemu ya barua ya umoja huo kwa
Zitto.
RUMAKO ni Ushirika wa Msingi wa Vijiji vya
Mkabogo, Rusaba na Matyazo wilayani Kigoma Vijijini ambako zaidi ya wakulima
wake 750 wameingia kuwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)
katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Kwa takribani miaka minne sasa, Zitto amekuwa
akipigania wakulima wa Tanzania kupewa uanachama wa wa mifuko hiyo ili
kuwakwamua kiuchumi na pia kuwawezesha kupata huduma ya hifadhi kama ilivyo kwa
wafanyakazi katika sekta rasmi wanaopata huduma hizo.
Akizungumzia tuzo hiyo, Zitto alisema, "Nimeipokea
tuzo hii kwa unyenyekevu mkubwa. Naamini kuwa siku za usoni haki ya hifadhi ya
jamii kwa wananchi itakuwa ni haki ya kikatiba.”
Alisema nchi masikini zinapaswa
kuongeza uwekaji akiba ili ziweze kuendelea kwa kasi kwani bila akiba uwekezaji
unakuwa mdogo na hatimaye uchumi haukui.
ECASSA ni umoja unaounganisha
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii takribani 20 katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda,
Rwanda, Burundi na Zambia.
0 Comments