Na Mwantanga Ame
MSWADA wa sheria itakayowabana
viongozi wa umma watakaokiuka maadili, unatarajiwa kuwasilishwa katika kikao
kijacho cha Baraza la Wawakilishi, imefahamika.
Sheria hiyo itaanzisha Tume ya
Maadili ya Viongozi wa Umma, ambapo pamoja na kazi nyengine, itakuwa na mamlaka
ya kuwabana viongozi wa umma kuhakikisha wanasalimisha mali zao.
Kikao hicho kinatarajiwa
kufanyika Oktoba 22 mwaka huu, ambapo Baraza la Wawakilishi limewataka wananchi
kuuchangia kabla ya kuwasilishwa kwa wajumbe.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa na Ofisi ya Baraza la Wawakilishi na kuthibitishwa na Ofisa
Uhusiano wa Baraza hilo, Himidi Choko, serikali imeamua kuwasilisha mswada huo
ambao utasimamia maadili ya viongozi wote watakaotajwa kwenye jadweli la mswada
huo.
Sheria hiyo itampa mamlaka
Mwenyekiti wa Tume kumtaka kiongozi wa umma kuwasilisha kwake tamko la
maandishi kuhusu mali anazomiliki.
Mbali ya mali zake, pia
kiongozi atalazimishwa kutaja mali zinazomilikiwa na wakala wake, madeni anayodaiwa
pamoja na mali na madeni ya mke au mumewe,watoto wao au watoto walio chini ya
uangalizi wao.
Aidha Tume itakuwa na uwezo wa kupokea
tuhuma na taarifa za uvunjwaji wa maadili kutoka kwa wananchi kwa kiongozi
yoyote wa umma, kufanya uchunguzi juu ya madai au tuhuma hizo.
Mswaada mwengine ambao
utawasilishwa unahusu mswada wa sheria ya kufuta sheria ya Wauguzi na Wakunga
(Uanzishwaji wa Baraza la Usajili wa Wauguzi na Wakunga) Nam. 9 ya mwaka 1986,
na kuanzisha badala yake sheria mpya ya wauguzi na wakunga na mambo
yanayohusiana na hayo.
Mswada huo unaanzisha Baraza la
Wakunga litakalokuwa na wajibu ya kusimamia fani ya wauguzi na wakunga.
Wananchi wametakiwa kuihangia
miswada hiyo ambapo tarehe ya mwisho ya kupokea maoni ni Oktoba 12 mwaka huu.
0 Comments