STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 08 Januari, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa Mashirika ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kushirikiana kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ili kuongeza kasi ya kuiletea maendeleo Zanzibar.
Dk. Shein ametoa wito huo leo wakati wa hotuba yake katika ufunguzi wa kiwanja cha kufurahishia watoto cha Uhuru kilichopo Kariakoo mjini Zanzibar ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kuadhimisha miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
“Wakati umefika sasa kwa taasisi zetu kama ZSSF, Shirika la Bima na Benki ya Watu wa Zanzibar kushirikiana na Serikali kutekeleza miradi mikubwa kama ambavyo taasisi kama hizo zinavyofanya huko Tanzania Bara” alisema Dk. Shein na kusisitiza kuwa “Zanzibar hatuwezi kushindwa kutekeleza mambo yetu ya msingi tukijidhatiti vya kutosha.”
Ujenzi wa kiwanja hicho ambao umefikia asilimia 90 unagharimiwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii Zanzibar-ZSSF na kugharimu jumla ya shilingi bilioni 15 utakapomalizika ni miongoni mwa miradi ya kibiashara inayotekelezwa na shirika hilo.
Miradi mingine ni mradi wa ujenzi wa Mnara wa Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi na ujenzi wa Kituo cha maduka makubwa ya biashara (Shopping Malls)katika eneo la Michenzani mjini hapa.
Katika halfa hiyo iliyohudhuriwa pia na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Dk. Shein alilipongeza Shirika la ZSSF kwa kuonesha njia katika kuwekeza kwenye miradi yenye faida za kiuchumi na kijamii hivyo kuchangia kuharakisha maendeleo ya Zanzibar.
Alieleza kuwa shilingi bilioni 15 zilizotumika katika kujenga kiwanja hicho zingeweza kutumika katika miradi mingine katika sekta kama za elimu na afya lakini Serikali iliona ni busara kutumia kiwango hicho cha fedha kwa ajili ya maslahi ya watoto lakini kwa kuliomba Shirika la ZSSF kutekeleza mradi huo kwa fedha zake na kuuendesha mradi huo kibiashara.
Dk. Shein alibainisha kuwa uamuzi huo unatokana na kuzingatia ukweli kuwa watoto ni sehemu ya maisha ya kila siku ya mwanadamu na ni sehemu maalum ya jamii na ndio maana serikali imetunga sera na sheria ya hifadhi ya watoto.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliutaka uongozi wa ZSSF kuangalia uwezekano wa kurejesha fedha za mradi kabla ya miaka kumi iliyojipangia na kupata faida mapema ili fedha hizo ziweze kutumika katika miradi mingine.
Aliwahakikishia wanachama wa mfuko huo wa jamii kuwa “fedha zao ziko salama na wasiwe na wasiwasi wa uwekezaji huo na kwamba wastaafu watapata mafao yao kama yalivyopangwa”
Aliwahakikishia pia wageni na wananchi waliohudhuria hafla hiyo kuwa serikali itaendelea na utekelezaji wa dhamira yake ya kubadili haiba ya mji wa Zanzibar na kuongeza kuwa uzinduzi wa kiwanja hicho ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira hiyo.
Katika hotuba yake hiyo Dk. Shein alitoa wito kwa wazazi wa kike na kiume kujenga ushirikiano katika kuwatembeleza watoto katika sehemu za michezo kama katika kiwanja hicho ili watoto waweze kufurahia na wazazi wao vyema.
“lazima tuwe na mapenzi na watoto wetu sote wazazi tushirikiane kuwatembeza watoto wetu tusiwaachie wazazi wa kike peke yao” Dk. Shein alisisitiza na kuongeza kuwa wakati wa kuwatembeza watoto wazazi hawana budi kuwaeleza watoto maana ya majina na maeneo ya historia katika sehemu wanazopita.
Mapema akimkaribisha mgeni Rasmi, Waziri wa Fedha Omar Yussuf Mzee alisema kuwa ili kuhakikisha kuwa viingilio vya michezo katika kiwanja hicho vinakuwa nafuu Serikali imetoa msamaha wa kodi kwa vifaa vyote vya michezo vilivyowekwa katika kiwanja hicho.
Alibainisha pia kuwa sheria ya manunuzi imefuatwa katika kutekeleza mradi huo huku akisisitiza kuwa zoezi la kuthamini thamani ya fedha za mradi litafanywa baadae na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali.
Katika maelezo yake ya awali Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF Bwana Abdulwakil Hafidh alieleza kuwa amefarijika kuona kuwa changamoto nyingi ambazo ziliukabili mradi huo zimepatiwa ufumbuzi kufuatia ziara ya Mheshimiwa Rais aliyoifanya mwezi April mwaka jana kuangalia maendeleo ya ujenzi wa kiwanja hicho.
Kuhusu huduma zinazopatikana katika kiwanja hicho bwana Abdulwakil alisema kuna jumla ya mapembea 12 ya kawaida na mengine 12 ya maji ambayo yako mbioni kufungwa, kutakuwa na michezo mbalimbali kwa video, jumla ya maduka 56 pamoja na kumbi za maonesho na shughuli nyingine za kijamii kama harusi.
Alibainisha kuwa ujenzi wa mradi huo ulioanza Oktoba 2012 umekamilika kwa asilimia 90 na asilimia iliyobaki ni ufungaji wa baadhi ya michezo na ukamilishaji wa baadhi ya majengo.
Aliwaeleza wageni na wananchi waliohudhuria hafla hiyo kuwa tayari Ofisi yake imeshafanya majaribio ya uendeshaji wa kiwanja hicho ikiwemo kuangalia mwenendo na udhibiti wa ukusanyaji wa mapato na uendeshaji wa michezo iliyopo.
Maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi yameanza tarehe 2 Januari, 2015 na yatafikia kilele chake tarehe 12 Januari, 2015 katika kiwanja cha Amaan ambako mgeni rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
0 Comments