6/recent/ticker-posts

Zoezi la utambuzi wa Wazee laanza

 Na Ramadhan Ali, Maelezo
 
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na watoto inaandaa zoezi la utambuzi wa wazee wenye umri  kuanzia miaka 60 na kuendelea ili kutambua  sehemu wanazoishi na kuwaandalia mazingira mazuri ya maisha yao.
 
Akizungumza katika mkutano wa Kamati Tendaji ya Mpango huo katika Wizara ya Uwezeshaji Mwanakwerekwe, Mkuu wa kitengo cha Hifadhi ya Jamii Zanzibar Salum Rashid amesema zoezi hilo litafanywa  katika shehia zote za Zanzibar.
 
Amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba baada ya wazee hao kutambuliwa watapewa kadi maalum ambazo zitawasaidia kwenye huduma muhimu za msingi za kijamii zinazotolewa na Serikali  zikiwemo usafiri na matibabu bila malipo.
 
“Lengo ni kuwaoredhesha wazee wote waliofikia umri kuanzia miaka 60  hapa Zanzibar kujua idadi yao kijinsia, Wilaya na Shehia zao na kuwapa vitambulisho  maalum vikavyowawezesha kupata huduma muhimu za kijamii bila malipo” alisisitiza Mkuu wa Kitengo cha Hifadhi ya Jamii.
 
Salum amesema maandalizi ya zoezi hilo yako katika hatua nzuri na litafanywa kwa uangalifu mkubwa ili  kuhakikisha kila aliefikia umri huo aweze kuoredheshwa kupitia shehia wanazoishi.
 
Katika kufanikisha mpango huo Wizara itaandaa vijana  wasiopungua 45 na kuwapa mafunzo  ya kazi hiyo  na  kila shehia itakuwa na kijana mmoja ambae atashirikiana na  sheha ama mjumbe wake.
 
Amesema kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 Zanzibar inaowazee 58311 wenye umri wa  kuanzia miaka 60  ambao ni sawa na asilimia 4.5 ya wananchi wote.
 
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na  Shirika la HelpAge mwaka 2009, asilimia 60 ya  wazee wenye umri huo hawana kipato rasmi cha kuendeleza maisha yao  na baadhi yao wamekuwa wakipata msaada mdogo kutoka kwa jamaa zao.
Amesema kutokana na usumbufu wa maisha unaowapata wazee hao ndipo Serikali ikaamua kuandaa mpango huo ili waweze kupatiwa msaada.
 
Akizungumza katika mkutano huo Naibu Katibu Mkuu  Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Msham Abdalla Khamis amesema  zoezi hilo halina uhusiano wowote na masuala ya siasa hivyo amewataka wananchi wasiwe na wasi wasi .
 
Amesema utaratibu kama huo wa  kuwatunza na kuwasaidia wazee unafanyika katika nchi nyingi duniani na umekuwa na mafanikio makubwa kwao.
 
Aidha amesema lengo kuu la  mpango huo ni kuwatambua wazee sehemu wanazoishi  ili kuwasaidia  waweze kujikimu kimaisha na kuwapatia baadhi ya huduma muhimu za kijamii bila malipo.
                                    Mwisho
 
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.

Post a Comment

3 Comments

  1. Kwa sababu Msham nae sasa ni mzee

    ReplyDelete
  2. Hili jambo kama litatimizwa basi hakika mtafanya jambo la maana na muhimu sana na hapo ndipo tutakubali kama SMZ yetu inajali raia wake kwa vitendo. Mungu wape usahau wote wenye dhamira mbaya kwa Zanzibar na Africa kwa ujumla, Wenu mkosha vizee vya kizungu UK

    ReplyDelete
  3. propaganda tu za kutaka kura uchaguzi ujao , tangu lini smz ikajali raia wake? wasingeuza nchi kwa watanganyika kwa tamaa zao za kibinafsi , huu ni ukweli na kawaida unauma ,

    ReplyDelete