Na Ramadhan Ali, Maelezo
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na watoto inaandaa zoezi la utambuzi wa wazee wenye umri kuanzia miaka 60 na kuendelea ili kutambua sehemu wanazoishi na kuwaandalia mazingira mazuri ya maisha yao.
Akizungumza katika mkutano wa Kamati Tendaji ya Mpango huo katika Wizara ya Uwezeshaji Mwanakwerekwe, Mkuu wa kitengo cha Hifadhi ya Jamii Zanzibar Salum Rashid amesema zoezi hilo litafanywa katika shehia zote za Zanzibar.
Amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba baada ya wazee hao kutambuliwa watapewa kadi maalum ambazo zitawasaidia kwenye huduma muhimu za msingi za kijamii zinazotolewa na Serikali zikiwemo usafiri na matibabu bila malipo.
“Lengo ni kuwaoredhesha wazee wote waliofikia umri kuanzia miaka 60 hapa Zanzibar kujua idadi yao kijinsia, Wilaya na Shehia zao na kuwapa vitambulisho maalum vikavyowawezesha kupata huduma muhimu za kijamii bila malipo” alisisitiza Mkuu wa Kitengo cha Hifadhi ya Jamii.
Salum amesema maandalizi ya zoezi hilo yako katika hatua nzuri na litafanywa kwa uangalifu mkubwa ili kuhakikisha kila aliefikia umri huo aweze kuoredheshwa kupitia shehia wanazoishi.
Katika kufanikisha mpango huo Wizara itaandaa vijana wasiopungua 45 na kuwapa mafunzo ya kazi hiyo na kila shehia itakuwa na kijana mmoja ambae atashirikiana na sheha ama mjumbe wake.
Amesema kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 Zanzibar inaowazee 58311 wenye umri wa kuanzia miaka 60 ambao ni sawa na asilimia 4.5 ya wananchi wote.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la HelpAge mwaka 2009, asilimia 60 ya wazee wenye umri huo hawana kipato rasmi cha kuendeleza maisha yao na baadhi yao wamekuwa wakipata msaada mdogo kutoka kwa jamaa zao.
Amesema kutokana na usumbufu wa maisha unaowapata wazee hao ndipo Serikali ikaamua kuandaa mpango huo ili waweze kupatiwa msaada.
Akizungumza katika mkutano huo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Msham Abdalla Khamis amesema zoezi hilo halina uhusiano wowote na masuala ya siasa hivyo amewataka wananchi wasiwe na wasi wasi .
Amesema utaratibu kama huo wa kuwatunza na kuwasaidia wazee unafanyika katika nchi nyingi duniani na umekuwa na mafanikio makubwa kwao.
Aidha amesema lengo kuu la mpango huo ni kuwatambua wazee sehemu wanazoishi ili kuwasaidia waweze kujikimu kimaisha na kuwapatia baadhi ya huduma muhimu za kijamii bila malipo.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.
3 Comments
Kwa sababu Msham nae sasa ni mzee
ReplyDeleteHili jambo kama litatimizwa basi hakika mtafanya jambo la maana na muhimu sana na hapo ndipo tutakubali kama SMZ yetu inajali raia wake kwa vitendo. Mungu wape usahau wote wenye dhamira mbaya kwa Zanzibar na Africa kwa ujumla, Wenu mkosha vizee vya kizungu UK
ReplyDeletepropaganda tu za kutaka kura uchaguzi ujao , tangu lini smz ikajali raia wake? wasingeuza nchi kwa watanganyika kwa tamaa zao za kibinafsi , huu ni ukweli na kawaida unauma ,
ReplyDelete