6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR- UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI CHUO CHA MAAFISA WA UHAMIAJI- KITOGANI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiweka jiwe la msingi la jengo la Chuo cha Mafunzo cha Idara ya Uhamiaji Zanzibar kilichopo Kitogani, Mkoa wa Kusini

Kuanzishwa kwa chuo cha mafunzo cha Idara ya Uhamiaji Zanzibar ni hatua muhimu katika kuwaongezea uwezo wa kitaalamu, kiutendaji na kimaadili Maafisa na askari wa Idara ya Uhamiaji Tanzania.
 

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la msingi la chuo cha Mafunzo ya Idara ya Uhamiaji Kitogani, Mkoa wa Kusini Unguja.    

Amesema kupitia chuo hicho Maafisa wa uhamiaji wateweza kujengewa uwezo katika masuala ya udhibiti wa mipaka, usalama wa Taifa, matumizi ya teknolojia, sheria za uhamiaji na kuheshimu haki za binaadamu jambo ambalo litaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kulinda maslahi ya nchi.

Mhe Hemed ameuagiza uongozi wa Idara ya uhamiaji kwamba chuo hicho kisiwe kwa ajili ya kutoa mafunzo ya awali pekee bali kitoe mafunzo ya mara kwa mara kwa maafisa, kufanya tafiti, kubadilisha uzoefu na Mataifa mengine duniani ili Idara ya Uhamiaji iendelee kuongeza hadhi zaidi katika masuala ya kiuhamiaji kwa ngazi ya Kikanda na Kiamtaifa.

Ameutaka Uongozi na Maafisa wa Idara ya Uhamiaji kuhakikisha nchi inakuwa salama dhidi ya wahamiaji haramu sambamba na wageni wanaoingia na kutoka kuendelea kufurahia huduma zinazotolewa na Idara hio kupitia mifumo ya kidijitali ili kurahisisha utoaji wa huduma mbali mbali kwa wageni na wanyeji wanaofika kwa ajili ya kupata huduma mbali mbali.

Hata hivyo, Makamu wa Pili wa Rais wa amemtaka mkandarasi na msimamizi wa chuo hicho kuhakikisha ujenzi huo unazingatia viwango vya ubora vinavyokubalika pamoja na kukamilika kwa wakati ili kutoa huduma kama kilivyokusudiwa.

Nae Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Mhe. George Simbachawene(MB)  amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kuendelea kuiimarisha Idara ya uhamiaji ili kuwa na hadhi ya Kitaifa na Kimataifa katika utoaji wa huduma zilizo bora kwa wananchi na wageni wanaoingia nchini..

Mhe. Simbachawene amesema Idara ya uhamiaji inaendelea kuimarika katika utoaji wa huduma kwa kutumia mifumo ya kielektroniki katika utoaji wa paspoti, uombaji wa vibali, ulinzi, udhibiti wa mipaka na wahamiaji haramu pamoja na kuongeza wigo wa makusanyo ya mapato yasiyotokana na kodi.

Aidha Mhe. Simbachawene ameahidi kusimamia vyema ujenzi na uendeshaji wa chuo hicho ili kiweze kuzalisha wataalamu wenye ujuzi, nidhamu na weledi katika kutekeleza majukumu yao ikiwemo ulinzi wa mipaka na utoaji wa huzuma bora kwa wannachi.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Ndugu Hassan Ali Hassan ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupatiwa boti kwa ajili ya kufanyia doria baharini ambayo itasaidia kudhibiti mipaka ya baharini, kudhibiti wahamiaji haramu pamoja na kufanya doria za visiwani kwa lengo la kuhakikisha usalama na utulivu kwa watalii wanaofika visiwani humo.

Kamishna Hassan amefahamisha kuwa Idara ya Uhamiaji inajipanga kuhakikisha kuwa kabla Serikali ya awamu ya nane kumaliza muda wake Idara ya Uhamiaji Zanzibar imekamilisha ujenzi wa Ofisi zake kwa Mikoa na Wilaya zote za Zanzibar ili kuimarisha utendaji kazi kwa Maafisa wa Uhamiaji.

Amesema kukamilika kwa ujenzi wa chuo hicho kutaleta mageuzi makubwa Zanzibar kwa kuwa chachu ya kuboresha mashirikiano ya kiutandaji nadani na nje ya nchi.

Akisoma taarifa ya kitaalamu juu ya ujenzi wa chuo hicho, Katibu Mkuu Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratib na Baraza la Wawakilishi Dkt. Islam Seif Said amesema ujenzi wa jengo hilo umetekelezwa kwa kuzingatia taratibu zote za kisheria uliogharimu shilingi za Kitanzania zaidi ya Bilioni kumi na mbili ambalo litalaza wanafunzi 320 kwa kila jengo na kwenda kutatua changamoto ya maeneo ya kufanyia mafunzo na kupatikana mazingira mazuri na salama ya kuishi maafsa wanapokuwa mafunzoni.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kutenga fedha za mgao zinazotokana na makusanyo ya Idara ya Uhamiaji ili kuweza kutekeleza Miradi mbali mbali ya maendeleo itakayorahisisha utowaji na upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Chuo cha Mafunzo cha Idara ya Uhamiaji kimejengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia fedha za makusanyo ya ndani ya Idara ya Uhamiaji na kuwa chuo cha Kwanza cha Idara ya Uhamiaji Zanzibar tangu kufanyika kwa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.

 

Imetolewa na Kitengo Cha Habari ( OMPR )

Leo tarehe 08 / 01 / 2026

Post a Comment

0 Comments