Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said S. Mussa, ametembelea Maonyesho ya 12 ya Biashara Zanzibar (ZITF) yanayoendelea katika Viwanja vya Nyamanzi, Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Balozi Mussa alipokelewa katika banda la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kaimu Mkurugenzi wa Ofisi ya Wizara Zanzibar, Bw. Ali S. Ali, pamoja na maafisa wa wizara hiyo, ambapo alipata fursa ya kujionea shughuli na huduma zinazotolewa na wizara kupitia maonyesho hayo.
Akizungumza katika banda hilo, Balozi Mussa aliwataka maafisa wa wizara kutumia kikamilifu jukwaa la maonyesho hayo kuelimisha wananchi kuhusu majukumu na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na wizara, hususan katika nyanja za diplomasia ya uchumi, ushirikiano wa kimataifa, biashara na uwekezaji, pamoja na kuonesha fursa zinazoweza kuchangia maendeleo ya taifa.
Katika ziara hiyo, Balozi Mussa alitembelea pia mabanda ya taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali, ikiwemo Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar, Ofisi ya Makamu wa kwanza Rais Zanzibar, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar na Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
Maonyesho ya 12 ya ZITF yalianza rasmi Disemba 29, 2025 na yanatarajiwa kuhitimishwa Januari 16, 2026.
0 Comments