Habari za Punde

SMZ YAKATAA MAFUTA KUWA YA MUUNGANO

Yaeleza kufanya hivyo ni kukiuka Katiba

Yasema ikikubali inakosa kiasi kikubwa cha mapato

Na Mwantanga Ame - Zanzibar leo


SERIKALI ya Zanzibar imeyakataa mapendekezo ya Mshauri mwelekezi katika suala la udhibiti na uendeshaji wa shughuli zinazohusiana na utafiti na uchimbaji mafuta na gesi asilia kuwa ni ya Muungano na badala yake suala hilo liwe ni la Zanzibar pekee.

Mapendekezo hayo yametolewa jana mbele ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Maji, Ujenzi Nishati na Ardhi, Mansoor Yussuf Himid, alipowasilisha taarifa ya serikali juu ya mapendekezo ya uendeshaji wa kazi za utafiti na uchuimbaji mafuta na gesi asilia Zanzibar.

Waziri Mansoor alisema serikali kwa kuzingatia mambo mbali mbali yaliyomo katika miongozo ya Katiba ya Zanzibar inaliona suala hilo halipaswi kuwa la Muungano na haikubaliani na ushauri wa Mtaalam muelekezi alioutoa.

Alisema pindipo serikali ikikubali kulifanya suala hilo kuwa ni la Muungano itakwenda kinyume na Katiba ya Zanzibar, kwa vile imeonesha kuwa suala la mafuta linavyoendeshwa sasa linakiuka Katiba.

"Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar sura ya kwanza kifungu cha 2.(1) kinafahamisha kuwa Ardhi na bahari ya ndani ya Zanzibar (terrtorrial Water) , maeneo ambayo usimamizi, udhibiti wa shughuli zianazohusiana na utafiti uchimbaji wa mafuta na gesi asilia uwe ni wa Zanzibar pekee kama katiba yetu na matakwa ya Wazanzibari yanavyoelekeza", alisema Mansoor.

Alisema, kwa hoja hiyo serikali inapata nguvu kwa kuzingatia kuwa suala la mafuta kama yalivyoelekezwa na Mshauri mwelekezi kwamba yanaweza kusababisha uharibifu mkubwa wa eneo la visiwa vya Zanzibar na kuwapo kwa hilo watakaoathirika ni wananchi wa Zanzibar.

Alisema suala hilo ni jambo zito na ni lenye hatari kubwa pindipo serikali ya Zanzibar itaamua kulikabidhisha kwa taasisi yoyote ya nje ya nchi kama inavyojitokeza hivi sasa katika Mkataba wa Antrim ambao haukuihusisha serikali ya Zanzibar.

"Vyenginevyo itakuwa tumekabidhi mustakabali wa Zanzibar katika mikono ya wizara ya Nishati na Madini inayosimamiwa na Waziri aliye nje ya Mamlaka ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar" alisema.

Alifahamisha kuwa kutokana na hali hiyo ni vyema suala hilo likaangaliwa ikiwa pamoja na kuitazama mifano ya nchi zenye Muungano uliofanana kutokana na ushauri ambao aliutoa muelekezi huyo.

Alisema serikali inashauri kwamba hivi sasa wakati umefika kwa Zanzibar kuwa na chombo chake cha kusimamia mambo yanayohusiana na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia na yanayoambatana nayo ambacho kitakuwa kama kile kilichopo sasa katika serikali ya Muungano cha TPDC.

Alieleza hiyo ndio njia pekee itakayoondosha migongano ya madaraka na maslahi na pia ni njia pekee ya kuhakikisha haki za Zanzibar na watu wake zinalindwa kwa sasa na hapo baadaye.

Akizungumzia kwa upande wa Bahari Kuu, alisema serikali inawashauri wajumbe wa Baraza hilo kukubaliana kuwa lindeshwe kwa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Hata hivyo, alieleza wakati hilo wakilikubali uendeshaji wake usiwe unafanyika kwa muundo uliopo sasa wa taasisi na sheria na iwe Zanzibar inakuwa ni mshiriki atakaepata haki sawa kulingana na makubaliano ambayo yatakuwa yamefikiwa katika eneo hilo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Ili kugharamia shughuli za Muungano, utaratibu wa kuchangia kama unavyoendeshwa sasa uendelee na kila upande ulazimike kuchangia kwa kiwango kile kile kitakachokubalika kwa thamani aidha ya fedha taslim au kiwango cha mafuta chenye thamani" alisema.

Alisema katika mapendekezo hayo ya serikali, ilizingatia katika maeneo matatu likiwemo la mikataba na aina ya mikataba, kodi za mapato, kodi ya ardhi, mafuta yatakayozalishwa, mafuta yatayofidia gharama, mafuta yatayobakia kuwa faida, mrahaba na mazingira.

Akitaja sababu zaidi za msingi ambazo serikali imezizingatia na kuliona suala la hilo kubakia kuwa ni la Zanzibar, Waziri Mansoor alisema serikali inaikosoa ripoti hiyo kwa kushindwa kuyaelewa bayana baadhi ya maeneo ambayo uendeshaji wake haiwezekani kuwemo katika mambo ya Muungano.

Akitoa mfano alisema suala la Ardhi si miongoni mwa mambo yaliomo katika Muungano na kutokana na hilo serikali zote mbili zimekuwa zikitumia sheria zake za kusimamia ardhi.

Kutokana na mfano huo alisema suala la mafuta na gesi asilia ni moja ya raslimali zinazopatikana chini ya ardhi pekee iwe iliyofunikwa kwa maji ama nchi kavu na kifungu cha 4 cha sura ya kwanza ya Katiba ya Zanzibar kinaipa nguvu serikali ya Zanzibar katika kutawala mambo ya ndani ya nchi.

Alisema sheria ambazo zinapaswa kurekebishwa ikwa suala hilo litaendeshwa kwa sura ya Muungano sio ya kusimamia mafuta pekee ambapo serikali italazimika kufanya marekebisho ya katiba huku ikizibadili sheria za Mazingira, usajili wa Makampuni, Misitu, Bodi za Mapato, Ajira, Bima, Uvuvi na bahari Kuu, na ya Nishati.

Alisema katika Katiba ya Zanzibar imeeleza wazi katika kifungu chake cha 10 (3), Kwamba serikali ya Zanzibar ndio itadhibiti Uchumi wa nchi kwa kufuata madhumuni yaliomo ndani yake likiwemo suala ala utoaji wa huduma bora na ili matakwa hayo yatekelezwe usimamizi wa raslimali moja kwa moja uwe mikononi mwa serikali ya Zanzibar.

Alisema kutokana na mapendekezo ya mshauri huyo kuhusu suala hilo ni wazi kuwa vipengele hivyo vya Katiba vikikiukwa hayo hayataweza kutekelezeka na kunauwezekano wa kuzuka kwa migongano ya Katiba mbili.

Alifahamisha kuwa hali hiyo inaweza ikatokea kutokana na kuwa ripoti ya Mshauri imelenga zaidi suala la mafuta kulibakisha kuwa ni la Muungano na ndio maana imeshauri kuwapo kwa mabadiliko kadhaa ya msingi ndani ya Taasisi za Muungano na Serikali ya Zanzibar.

Alisema serikali haikubaliani na ushauri huo kutokana na kuwa muelekezi huyo ameshindwa kubaini kwamba Tanzania ina katiba mbili ambazo zinatakiwa kuoana na sio kukizana.

"Ushauri wa ripoti hii ukitekelezwa utaishia kwenye mgongano mkubwa wa kikatiba, sheria, kiuchumi na kijamii, tutajikuta tunarejea kwenye mtihani wa kutaka kulifumbua tatizo hili kwa maridhiano ya dharau badala ya makubaliano ya kudumu" alisema Waziri huyo.

Waziri huyo alifahamisha kwamba kuyakubali mapendekezo ya mshauri huyo ni moja ya mtego thakili unaoikabili serikali na suala hilo linaweza kubakia kuwa ni historia kwa vile ripoti hiyo imetoa mapendekezo ambayo yanazungumzika katika pande zote mbili.

"Ripoti hii imeangalia zaidi katika katiba ya Muungano wa Tanzania kuliko ile ya Zanzibar, naishia kuifananisha ripoti hii na mapendekezo yake kuwa kama jahazi iliyochongwa ikachongeka lakini ikachelezwa kwenye kina kifupi cha maji kuliko uzito wake, itabidi kuwa na mfano wa jahazi lakini haitamvusha yoyote kuelekea hatma ya safari yake" alisema waziri.

Alisema haiwezekani kwa serikali kufuata ushauri huo ambao utakuwa ni kinyume kwani lazima wafahamu umuhimu wa kuwapo kwake na haiwezekani ikaachiwa, kwa vile Katiba ipo kuwatumikia watu na sio watu waitumikie Katiba, na pindipo ikifikia hapo kutahitaji kufanyiwa marekebisho na bila ya hivyo kunaweza kusababisha mtafaruku mkubwa.

Alizitaja athari ambazo zitaweza kutokea Waziri huyo alisema ikiwa serikali itakubali suala hilo kuwa ni ya Muungano baada ya maoni ya mwelekezi ni pamoja na kukosa mapato ya Muungano yanayo kusanywa kwa hali ya sheria ya sasa hubakia katika serikali ya Muungano.

Alisema kwa upande wa Mashirika kodi ya Mapato kwa Kampuni huwa inalipwa pale kampuni inaposajiliwa makao makuu yake ambapo kutokana na ushauri wa Muelekezi ameeleza kuwa mapato yatalipwa tanzania bara na hivyo kutochangia chochote katika mfuko wa serikali ya Zanzibar.

Hasara nyengine ambayo Zanzibar itaipata ni katika kodi ya mishahara ya wafanyakazi ambayo yatalipwa Tanzania bara kwa kila mwezi kama inavyojionesha katika taasisi za BOT, JWTZ, Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa.

Kodi nyengine ambayo itakosekana kwa Zanzibar ni ya Makampuni yatakayopewa leseni ambapo usajili wake utalazimika kusajiliwa Tanzania bara, na kukosekana kwa kodi hizo kukusanywa Zanzibar kutakuwa ni moja ya kasoro kubwa katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na uchimbaji wa mafuta.

"Hali hii ndio inayotokea sasa kodi kubwa ya mishara ya wafanyakazi wa Muungano inakusanywa bara, wakati huku wafanyakazi hao wakitumia huduma za bure za matibabu maji, elimu, na baarabara" alisema waziri huyo.

Alifamaisha Zanzibar itakosa mapato yote yatokanayo na leseni na kodi na ushuru na ni sawa na inavyojitokeza sasa katika kampuni ya Zantel ambayo imekuwa ikilipa jumla ya dola za Marekani 3,000,000 ambazo ni sawa na shilingi 3,900,000,000 kila mwaka hulipwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kwa ajili ya utoaji wa leseni na Zanzibar haipati kitu.

"Hivi sasa Kampuni ya Zantel inalipa jumla ya dola za Marekani 200,000 sawa na shilingi 260,000,000 ikiwa ni malipo ya mrahaba ambayo inaenda tanzania bara na hili likikubalika basi mapato yatakuwa chini ya TPDC" alisema Waziri huyo

Aidha Waziri huyo alisema kuwa suala hilo kufikishwa katika mamlaka hiyo ya mafuta Tanzania halikuwa ni maridhiano kama sheria za bunge zinavyoelekeza kutaka lazima liridhiwe na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Kutokana na hali hiyo, alisema ni wazi kuwa suala hilo linafanyika isivyohalali huku Zanzibar ikiwa haifaidiki na aina yoyote ya madini yakiwemo ya dhahabu, almasi na gesi.

Waziri huyo aliwataka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuichambua kwa kina ripoti hiyo ili kuiwezesha serikali ya Zanzibar kufaidika na suala hilo huku ikijenga mazingira bora ya ustawi wa jamii ya Wazanzibari

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi jana jioni walianza kujadili ripoti hiyo ambayo mjadala wake utaendelea hadi Jumatatu.






No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.