Asema dhambi ya uroho wa madaraka yausumbua upinzani
Na Mwanajuma Abdi
MGOMBEA wa Urais wa Zanzibar kwa Chama cha Alliance for Tanzania Farmers Party (AFP), Said Soud Said amesema vyama vya upinzani ikiwa vitaendelea kung'ang'ania uroho wa madaraka huku vikikataa kuungana havitaweza kukishinda Chama cha Mapinduzi.
Alisema wapinzani wasijidanganye, mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohammed Shein atashinda katika uchaguzi kwa vile atapata kura nyingi kuliko wagombea wa upinzani.
Soud alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Afisi za Chama cha NCCR Mageuzi Mwanakwerekwe mjini hapa, ambapo mkutano huo pia uliwahusisha wagombea wa Urais wa Chama TADEA, Juma Ali Khatib na Mgombea Mwenza wa Chama cha NCCR Mageuzi, Ali Omar.
Alisema siku itakayotokea vyama hivyo vimeungana kwa kusimamisha mgombea mmoja ndipo watakapoweza kuigaragaza CCM lakini bila hivyo chama hicho tawala kitashinda kama kumsukuma mlevi.
Mgombea huyo alimshutumu vikali Hamad Rashid wa CUF kwa kuwaita mabilisi baadhi ya wagombea wa vyama hivyo, kauli ambayo ameilaani huku akisema kila Mzanzibari ana haki ya kikatiba na sheria kugombania nafasi yeyote ikiwa anazo sifa.
"Hii ni nchi ya watu wote, hakuna mtu mwenye hatimiliki hapa wala hakuna chama chenye hatimiliki na kama CUF wana nguvu si wangalikwishachukua serikali, wanaacha kunadi sera wasema kuna vyama vinawaharibia kura", alisema Soud.
Alisema ni heri ya bilisi akisemeshwa anasikia kuliko mashetani ambao lazima wapate damu kila baada ya miaka mitano na ndio maana wanafanya vurugu za kukataa matokeo.
Alisem Chama cha CUF, kimeshapoteza muelekeo kutokana na watu wake wengi kutojiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura hasa kisiwani Pemba kutokana na Maalim Seif kuwakataza wasijiandikishe.
Nae Mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa Chama cha TADEA, Juma Ali Khatib aliliomba jeshi la Polisi kuwapatia ulinzi wagombea wa vyama vyote majumbani na sio kwa vyama viwili kwani nao wanaweza kupata matatizo hususan katika kipindi hiki cha kampeni.
Aidha alitoa wito kwa vyombo vya habari vya Umma kufuata maadili ya kazi zao kwa kuweka usawa kwa vyama vyote katika kuonesha na kutangaza mikutano ya vyama vya siasa.
Alisema Chama hicho kikishika madaraka watafanya mageuzi makubwa katika vyombo hivyo kutokana kutoa taarifa zake kwa upendeleo.
Hata hivyo, wagombea hao wote kwa pamoja wamewaomba wahisani wa washirika wa maendeleo wakiwemo UNDP kuviwezesha vyama vidogo kifedha ili viweze kumudu harakati za kampeni.
Walifahamisha kuwa, wagombea wa vyama hivyo wanashindwa kwenda kuwafikia wananchi kwa vile hawana vyombo vya usafiri kutokana na baadhi yao wanafanya kampeni kwa baskeli na pikipiki wakati vyama vyengine vina usafiri wa helikopta na magari makubwa.
0 Comments