6/recent/ticker-posts

DK SHEIN AAHIDI KUZIIMARISHA MASKANI ZA CCM

Na Rajab Mkasaba, Ikulu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein ameahidi kuziimarisha maskani za CCM ili ziimarike na ziendelee kukiletea ushindi Chama Cha Mapinduzi na viongozi wake.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa afisi ya CCM Mkoa wa Mjini Magharibi, wakati alipokuwa na mazungumzo na Wenyeviti na Makatibu wa Maskani za Mkoa wa Mjini Magharibi.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema kuwa Maskani za CCM na viongozi wake wamefanya kazi kubwa katika kukiletea ushindi Chama Cha Mapinduzi hivyo kuna kila sababu za kuziimarisha maskani hizo.

Dk. Shein alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi na viongozi wake ni lazima wahakikishe maskani zinaimarika kwani ni chimbuko na sehemu muhumu katika chama.

Alisema kuwa atajitahidi kwa kushirikiana na viongozi wenzake wa Chama katika kuhakikisha Maskani za CCM zinaimarika na kuweza kukiendeleza na kukipa ushindi chama hicho.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao wa CCM kuwa amani na utulivu iliyopo Zanzibar na hatua ya kufanya uchaguzi uliokuwa wa huru na haki umeweza kuijengea sifa kubwa Zanzibar.

Alisema kuwa hadi hivi Zanzibar imeendelea kumwagiwa sifa kutoka ndani na nje ya nchi kwa kuendesha uchaguzi kwa salama na amani sanjari na kuendeleza maelewano yaliofikiwa.

Dk. Shein alisema kuwa kutokana na hatua hiyo ipo haja ya kuendelea na kuisimania Ilani na Sera za CCM ili chama hicho kizidi kuimarika zaidi.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema kuwa wakati wa kampeni aliahidi na kusisitiza kuwa kampeni hizo zitafanyika kwa ustaarabu na ndivyo ilivyotokea na hatimae Chama Cha Mapinduzi kupata ushindi.

Kutokana na hatua hiyo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa wanamaskani na wanaCCM wote kwa kushirikiana na viongozi wao katika kufanya kampeni zilizokuwa za kistaarabu na kuweza kukipa ushindi Chama Cha Mapinduzi na viongozi wake.

Aidha, Dk. Shein aliwasisitiza wanaCCM na viongozi hao wa maskani kuwa umoja na mshikano wa wanaCCM unahitajika ili kukiimarisha chama hicho na kuendeleza amani na utulivu nchini.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwasisitiza wanaCCM kuendeleza umoja wao waliokuwa nao na wasikubali kuhadaiwa na kujiingiza katika mizozo.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwaeleza wanaCCM hao kuwa serikali anayoingoza inaenda vizuri na mashirikiano makubwa yamekuwepo kati ya viongozi wa serikali hiyo.

Dk. Shein alieleza kuwa Ilani ndio chimbuko la maendeleo hivyo serikali anayoiongoza inatekeleza Ilani hiyo kwa vitendo na hatua nzuri.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Mhe. Saleh Ramadhan Ferouz alimpongeza Dk. Shein kwa uwamuzi wake wa kwenda kuwashukuru na kuwapongeza viongozi wa maskani za Mkoa wa Mjini Magharibi.

Mhe. Ferouz alirejea kusema kuwa ahadi aliyoahidi Dk. Shein wakati wa kampeni kuwa kampeni zitafayika kwa ustaarabu imesihi na kumpongeza kwa mafanikio yaliopatikana ya kukipa ushindi Chama Cha Mapinduzi na kumchagua Dk. Shein kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na viongozi wengine wa CCM.

Aidha, Naibu Ferouz alitoa pongezi kwa Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Karume kwa kushiriki kikamilifu katika kampeni za uchaguzi za CCM na kuweza kukinadi chama hicho na hatimae kupata ushindi wa kishindo.

Viongozi mbali mbali wa CCM walihudhuria ambapo pia, katika mkutano huo vikundi mbali mbali vya ngoma za utamaduni na burudani vilitumbuiza

Post a Comment

0 Comments