Habari za Punde

WAGONJWA WA AKILI WAONGEZEKA KIDONGO CHEKUNDU

Na Halima Abdalla

KIASI ya wagonjwa wa akili 171 wamelazwa katika Hospitali ya Ugonjwa wa akili Kidongo Chekundu kuanzia Oktoba hadi Disemba mwaka jana, wakiwemo wanaume 71 na wanawake 100.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Muuguzi wa Afya ya Akili katika hospitali hiyo, Said Shaa Bakar, alisema tatizo linalosababisha ugonjwa huo kuzidi katika jamii ni utumiaji wa dawa za kulevya kwa upande wa wanaume.

Alifahamisha kuwa katika kipindi hicho, hospitali hiyo imekuwa ikipokea wagonjwa wengi wanaume wanaodaiwa kutumia dawa za kulevya.

Alisema kwa upande wa wanawake wengi wanaopata maradhi haya yanasababishwa na kuwa na tafrani za maisha pamoja na mawazo, ikiwemo kutelekezwa katika ndoa.

Aidha alifahamisha kuwa wengine wamekuwa wakipata maradhi haya kutokana na urithi kutoka kwa wazee pamoja na kupata kifafa.

Alifahamisha kuwa changamoto zinazoikabili hospitali hiyo na watumishi wake ni baadhi ya watu kuamini kuwa ugonjwa huo unasababishwa na shetani, hivyo wanapokuwa na mgonjwa wa aina hiyo huanza kumpeleka kwa waganga na wanaposhindwa huko ndio wanamkimbiza hospitalini hapo.

Alisema kinachoshangaza ni kuwa familia nyingi zinapopeleka watu wao katika hospitali hiyo baadae hukimbia hali inayosababisha kukosekana ushirikiano kati ya wanafamilia na hospitali hiyo.

Sambamba na hayo alisema changamoto nyengine iliyopo ni ukosefu wa dawa pamoja na uchache wa wauguzi kwani wauguzi waliopo kwa sasa ni kidogo.

Aidha, alisema idadi ya wagonjwa wanaohudhuria kliniki hiyo kwa ajili ya kupata dawa ni 2492 kati ya hao wanaume 1142 na wanawake1350.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.