RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kuleta maendeleo na kuhakikisha wananchi wa Bopwe wanapata maendeleo kama wananchi wa maeneo mengine hapa Zanzibar.
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa akiwahutubia wananchi mara baada ya kuifungua skuli mpya ya msingi ya Bopwe, iliyopo Jimbo la Gando, Mkoa wa Kaskani Pemba ambayo imejengwa kwa msaada wa Serikali ya Marekani.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa itahakikisha inawapelekea maendeleo wananchi wake wote, popote pale walipo bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
Alisema kuwa katika kuwapelekea maendeleo, serikali haitowasaidia wananchi wake kwa kuangalia ukabila, dini, rangi ama itikadi ya kisiasa na kusisitiza kuwa katika kuwapelekea maendeleo wananchi mambo hayo yote hayana nafasi.
Alisisitiza kuwa katika hatua hiyo maendeleo hayawezi kupatikanwa kama hapatakuwepo amani, utulivu, umoja na msikamano wa wananchi.
Dk. Shein alisema kuwa kwa upande wa Bopwe mafanikio yameweza kupatikana kwa kujengwa skuli hiyo ya kisasa iliyofadhiliwa na serikali ya Marekani kupitia ubalozi wake uliopo nchini kwa mashirikiano na Wanajeshi wa Marekani wanaofanya kazi Kanda ya Afrika wenye makao yao Djibouti.
Alisema kuwa ni lazima mashirikiano yawepo katika kujiletea maendeleo na kueleza kuwa Bopwe imeweza kufanikiwa katika ujenzi huo ambapo watoto wataweza kupata elimu itakayowasaidia katika maisha yao.
Alisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila ya kuwepo kwa elimu na kutoa shukurani kwa serikali ya Marekani kwa kusaidia ujenzi huo wa skuli ya msingi na kueleza kuwa serikali itaendelea kuwapelekea maendeleo wananchi hao ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara na huduma nyengine za kijamii.
Aidha, Dk. Shein aliwahimiza wazee, waalimu kushirikiana na serikali katika kuhakikisha watoto wanaenda skuli na kufuata taratibu za masomo na kuwapongeza waalimu kwa juhudi zao sanjari na pongezi kwa wananchi wa Bopwe kwa kuanza wenyewe ujenzi wa mradi huo wa skuli.
“Ukiwa na wazo zuri la maendeleo liendeleze”, alisisitiza Dk. Shein na kusema kuwa wazo la ujenzi wa skuli hiyo ni zuri ambalo mafanikio yake yameanza kuonekana akieleza pia na wazo ambalo wananchi hao wanalo la kuendeleza ujenzi wa skuli hiyo kwa kujenga jengo la ghorofa ni wazo zuri na kuahidi kuliunga mkono mara ujenzi utakapoanza.
Katika hotuba yake hiyo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa serikali ya Marekani kwa kusaidia miradi mbali mbali ya maendeleo pamoja na kuahidi kuendelea kuunga mkono zaidi miradi ya maendeleo hapa Zanzibar.
Alisema kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ambayo Marekani imeweza kuiunga mkono Zanzibar ni pamoja na mradi mkubwa wa umeme kutoka Dar-es-Salaam kwenda Unguja, msaada wa vitabu vya sayansi kwa wananfunzi wa sekondari, mradi wa kutumia compyuta kwa wananfunzi wa skuli za msingi za Unguja na Pemba na miradi mengineyo.
Alisema kuwa hatua hiyo inatokana na lengo la serikali la kuwasaidia wananchi katika kuwapelekea maendeleo sanjari na kutatua matatizo na changamoto wanazozikabili.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina changamoto kubwa katika kuwasaidia wananchi na kueleza kuwa viongozi waliowachagua watahakikisha wanafanya kazi kwa pamoja katika kuwatumikia wananchi hao.
Katika mazungumzo hayo pia, Dk. Shein aliupongeza uongozi wa Jimbo hilo la Gando kwa kushirikiana na wananchi katika kuwapelekea maendeleo na kutoa shukurani kwa Wizara, waalimu na wanafunzi na wazee wa Wilaya ya Wete kwa kuendeleza historia ya elimu katika Mkoa huo.
Akitoa mfano kwa Skuli ya Utaani, Dk. Shein alisema kuwa skuli hiyo iliyopo Wilaya ya Wete ina historia kubwa katika kutoa elimu na ndio maana serikali ikaamua kwa makusudi kuifanyia ukarabati mkubwa.
Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Ramadhan Abdalah Shaaban alitoa pongezi kwa serikali ya Marekani kwa misaada yao mbali mbali katika kuimarisha sekta ya elimu hapa Zanzibar ikiwa ni pamoja na msaada wa vitabu ambavyo vimechangia kwa kiasi kikubwa kupasisha wanafunzi wa sekondari.
Alieleza kuwa uwamuzi wa Marekani kusaidia waalimu watakao somesha skuli za chekechea kwa ajili ya kuwajengea uwezo kutokana na sera ya elimu ya kutaka elimu ya msingi ianzie chekechekea, msada huo utasaidia kwa kiasi kikubwa.
Nae Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe. Alfonzo Lenhardt, alisema kuwa serikali ya Marekani na wananchi wake wataendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha miradi ya maendeleo.
Balozi Lenhardt alieleza kuwa uwamuzi wa wazee na wananchi wa Bopwe wa kujenga skuli hiyo ulimpa moyo na kumshajihisha kwa kiasi kikubwa na ndio maana akafanya juhudi za kuhakikisha ujenzi huo unafanikiwa.
Balozi huyo alitoa pongezi kwa Rais Obama wa Marekani, Rais wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa dhamira zao za kuimarisha sekta ya elimu nchini Tanzania.
Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa inafanya kazi kubwa katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Balozi Lenhardt alisema kuwa Serikali ya Marekani itaendelea na juhudi zake za kuhakikisha inatoa mashirikiano mazuri kwa Zanzibar katika kuendeleza mustakabali mwema wa nchi.
Pamoja na hayo, Balozi huyo alitoa ahadi ya kusaidia kompyuta katika skuli hiyo sanjari na kueleza jinsi anavyovutiwa na juhudi za serikali katika muimarisha miradi yake ya maendeleo ikiwemo miradi elimu, ya ujenzi wa barabara, mawasilinao na miradi mengineyo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Abdalla Mzee alieleza kuwa skuli hiyo imejengwa kwa msada wa serikali ya Marekani kwa muda wa miezi sita ambayo tayari imeshaanza kusomesha wanafunzi wa msingi.
Alisema kuwa huo ni msaada wa pili katika kisiwa cha Pemba katika ujenzi wa skuli ambapo serikali ya Marekani pia, imesaidia ujenzi wa skuli ya Matale,iliyoko Mkoa wa Kusini Pemba.
Pia, alieleza kuwa katika uungwaji wake mkono kupitia Shirika lake la misaada la Marekani USAID limetoa msada wa madawati 60 katika skuli hiyo mpya ya msingi ya Bopwe.
Naibu Katibu Mkuu huyo, alisema kuwa katika Wilaya ya Wete kumekuwa na mashindano makubwa ya elimu katika kupasisha wanafunzi ambapo mwanafunzi bora wa mwaka huu wa kwanza na wa pili wametoka katika Wilaya hiyo.
Amesema kuwa skuli ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika Wilaya hiyo ni skuli ya Limbani, Jadida,Mitiulaya na Kizimbani ambazo mwaka huu zimeweza kutoa wanafuzi 237 wa michipuo ikilinganishwa na skuli nyengine 16 za Wilaya hiyo ambazo zimetoa wanafunzi 34.
Nao viongozi na wananchi wa Jimbo la Gando walitoa shukurani zao kwa Serikali ya Marekani kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuhakikisha ujenzi wa skuli hiyo unafanikiwa na kuweza kuwapunguzia masafa watoto ya kwenda kufuata elimu katika skulizilizopo mbali na makaazi yao.
Walieleza kuwa mashirikiano ya pamoja kati ya Wizara, wazee na viongozi yameweza kufanikisha mradi huo na kuahidi lengo lao la kujenga jengo la ghorafa katika skuli hiyo ili kuiimrisha zaidi na kuomba msaada wa kujenge kituo cha afya katika eneo lao hilo, ombi ambalo lilikubaliwa na Dk. Shein.
Zaidi Shilingi milioni 400, zimetumika katika ujenzi wa skuli hiyo ya msingi ya Bopwe, iliyopo Mkoa wa Kaskazini Pemba
No comments:
Post a Comment