Habari za Punde

MISHAHARA KUPANDA 2011/12

Na Ramadhan Makame, Mwanajuma Abdi

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar inalifanyiakazi suala la kuwaongezea mishahara watumishi wake ili waweze kumudu gharama za maisha.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee alieleza hayo alipokuwa akijibu suali lililoulizwa na Muwakilishi wa Jimbo la Ziwani, Rashid Seif Suleiman.

Katika suali lake la msingi, Mwakilishi huyo alitaka kufahamu serikali imejipanga vipi kwa bajeti inayokuja kuongeza mishahara ya watumishi angalau kufukia shilingi 200,000 kwa mwezi.

Waziri huyo alisema serikali inatambua udogo wa mishahara ya watumishi kulingana na hali ya maisha na inalifanyiakazi na kwamba imepanga kuongeza mishahara hiyo.

Alisema suala la kuwaongezea mishahara watumishi linategemea hali ya uchumi inaporuhusu na hasa kuongezeka kwa mapato ya serikali.

Aidha alisema suala la kupandishwa kima cha chini cha mishahara kitakapowadia muda wake litafanywa na Waziri wa anayeshughulikia masuala ya Utumishi wa Umma serikalini.

“Nisingependa kwa wakati huu kutaja kima cha chini cha mishahara kwa mwaka 2011/2012, kwani jukumu la kutaja kima cha chini ni la Waziri anayeshughulikia masuala ya Utumishi wa Umma Serikalini”, alisema Waziri huyo.

Waziri huyo akielezea kima cha chini cha mishahara kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka kwa kiwango cha dola za Marekani alisema kima cha chini cha mtumishi wa umma nchini Kenya anapokea dola 830, Rwanda dola 496, Tanzania Bara dola 1080 na Zanzibar ni dola 800 kwa mwaka.

Hata hivyo, aliwahakikishia wajumbe hao kwamba mishahara itakapoongezwa itazingatia maslahi bora kwa wataalamu ili waweze kubakia nchini kupitia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.