Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Dkt. Juma Malik Akili amesema kuwa kukusanya taarifa na kuzisambaza kwa njia ya kimtandao kutaifanya Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikari kupata mafanikio zaidi katika kazi zao za msingi za kitakwimu.
Dkt. Akil ameyasema hayo alipokuwa kwenye ziara ya kuitembelea Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ikiwa ni hatua ya kuzitembea Ofisi zilizo chini ya Wizara yake.
Amesema Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ni chimbuko la maendeleo ya Taifa kupitia Takwimu sahihi zinazozalishwa na ofisi hiyo kutumiwa na Serikali pamoja na watunga Sera mbali mbali nchini mwetu.
Hivyo ameisisitiza ofisi hiyo kuendelea kufanya kazi kwa ueledi pamoja na kuzingatia matumizi ya mifumo kwani itazidi kuleta chachu kwenye ukusanyaji na usambazaji wa tafiti mbali mbali.
Nae Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Hamad Omari ameishukuru Ofisi hiyo kwa kazi zake za kila siku ambazo zinawapa wananchi kutambua hali halisi ya mambo yanavyoendelea.
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Nd. Salum Kassim Ali alimueleza Mhe. Waziri kuwa Ofisi yake imekuwa ikikusanya Takwimu za kila Wizara ingawa bado kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya Wizara kutozitumia kikamilifu Takwimu hizo. Aidha, ameziomba Wizara hizo na taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali kutumia mfumo mpya wa ZANSIS ambao umekusanya aina zote za takwimu za hapa nchini.
Makamo Mwenyekiti wa Bodi ya Takwimu Dkt.Mary Mtumwa Khatib amesema Bodi inaridhishwa na kazi zinavyofanywa na ofisi hii na anaamini ikiwa Serikali na Taasisi binafsi wataendelea kutumia takwimu hizo basi itasaidia sana kwenye kupanga, kutunga Sera na kuchukua tahadhari ya yale tunayopaswa kuyaondosha nchini kwetu.





0 Comments