SHIRIKA la ‘Aide Medicate Development’ (AMD) la Ufaransa kanda ya Tanzania kwa kushirikiana na Jumuiya ya ZAYEDESA limekabidhi mashine ya Ultra Sound Scan, kwa Wizara ya Afya ambayo itasaidia kutoa huduma kwa mama wajawazito kwa vituo vya afya katika vijiji vya Unguja.
Mwakilishi wa shirika hilo kutoka Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Francois Leonardt alimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Mohamed Saleh Jiddawi, kwenye hafla iliyofanyika jana, katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja mjini hapa.
Mwakilishi huyo, alisema mashine hiyo itasaidia kuimarisha huduma za afya za akinamama wajawazito katika maeneo ya vijijini, ambapo kwa muda mrefu walikuwa wanaifuta mjini.
Alieleza msaada huo umetolewa na AMD kwa kushirikiana na Jumuiya ya ZAYEDESA ambao umekuwa wakifanya kazi karibu katika miradi mbalimbali ya kuimarisha huduma za akinamama wajawazito.
Nae Agnes Viellard kutoka Shirika la AMD Tanzania, alisema kutolewa kwa mashine hiyo itasaidia kuwasogezea huduma hiyo wananchi wa vijiji vya Unguja, kupitia katika vituo vya afya mbali mbali, ambapo kabla ya wataalamu kufika katika maeneo hayo kutatolewa matangazo ili kujuulishwa jamii.
Alifahamisha kuwa, shirika AMD na ZAYEDESA limekuwa likifanya kazi karibu miaka sita chini ya Mwenyekiti wake Shadya Karume kwa kusaidia mategenezo na uwekaji wa vifaa vya kisasa katika wodi za wazazi zikiwemo hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, Micheweni na Kivunge.
Aliongeza kusema kwamba, kifaa hicho kitafanya kazi ya kuchungua na kuonyesha ujauzito unavyoendelea, kutathmini hali ya mtoto tumboni na kumsaidia mama mjamzito kuweza kujiandaa kuzaa salama.
Nae Mwakilishi wa Jumuiya ya ZAYEDESA, Malik Mohamed Hanif alisema wanamashirikiano makubwa na shirika la AMD Tanzania kwa kufanya kazi pamoja, jambo ambalo limesaidia kupatikana kwa mashine hiyo waliyoikabidhi kwa ajili ya huduma za akinamama wajawazito katika vituo vya afya vijijini, ili wananchi wa huko wapate fursa hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Jiddawi alimshukuru mashirika hayo yasiyo ya kiserikali AMD na ZAYEDESA pamoja na serikali ya Ufaransa kwa misaada mbali mbali inayotolewa katika sekta ya afya hususani ya kuimarisha huduma za akinamama wajawazito.
Alisema msaada hiyo ilitolewa katika matengenezo makubwa ya Wodi ya wazazi Mnazimmoja, Micheweni, Tumbatu na Kivunge sambamba na uwekaji wa vifaa vya kisasa ili kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.
No comments:
Post a Comment