Habari za Punde

BARUA YA WAZI KWA WAJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI

Mheshimiwa Mjumbe wa BLW,

MUWAZA inakuandikia ukiwa kama mlinzi wa maslahi ya Zanzibar unayeumia katika moyo wako unapoona mamlaka ya kiutawala na kiuchumi ya Zanzibar yanadhoofika na kupotea kila siku kuelekea Tanganyika kwa kutumia jina la Tanzania.

MUWAZA inapata faraja kuona Baraza la Wawakilishi (BLW) la Zanzibar limeanza kutumia uwezo wake wa ki-katiba katika kutetea maslahi ya nchi yake. Katika BLW lililopita tulishuhudia uzalendo wa wajumbe pale walipolitoa suala la mafuta kutoka ndani ya mamlaka ya muungano. Baraza hilo pia liliwapa wananchi wa Zanzibar haki ya kuamua mambo mazito yanayohusu nchi yao kwa kupitia kura ya maoni.

Pia, BLW lililopita lilichukua hatua ya kuirekebisha katiba kwa kubainisha kwamba Zanzibar ni nchi pamoja na kuweka bayana mipaka yake. Hatua hiyo ilikuja baada ya Serikali ya Muungano kutangaza rasmi kwamba Zanzibar si nchi. Mambo haya ni mifano michache tu inayodhihirisha nguvu na uwezo wa ki-katiba wa BLW katika kutetea maslahi ya Zanzibar.

MUWAZA pamoja na Wazanzibari wengine tunaimani kwamba nguvu na uwezo wa BLW utaendelea kutumika ili kuinusuru Zanzibar. Imani hii inaongezeka kila tunapokumbuka kwamba Wazanzibari wameungana kisiasa kutokana na matunda makubwa ya BLW lililopita ya kupitisha sheria ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Katika waraka huu, MUWAZA ingependa kukutanabahisha juu ya tatizo sugu la muungano wa Zanzibar na Tanganyika. Ni jambo linalofahamika na kila mwenye kutaka kufahamu kwamba muungano huo uliodumu kwa miaka 47 sasa si wenye haki wala maslahi kwa Zanzibar.

Jee! Unafahamu kwamba muungano wa Tanzania ni wenye utata na usioeleweka kisheria wala kimantiki?

Jee! Unafahamu kwamba Tanganyika kwa kutumia jina la Tanzania imepiga hatua kubwa mbele katika maendeleo ya kiuchumi, miuondombinu, na utawala huku Zanzibar ikipigishwa hatua nyuma katika nyanja hizo?

Jee! Unafahamu kwamba Zanzibar imebanwa na kudumazwa katika mamlaka na maendeleo ya kiuchumi na kisiasa?

Jee! Unafahamu kwamba kabla ya muungano Zanzibar ilikuwa mbele zaidi katika nyanja za maendeleo ya uchumi, elimu, n.k. kuliko Tanganyika?

Jee! Unadhani Zanzibar ya leo haiwezi kujitawala yenyewe huku ikipiga hatua mbele katika maendeleo ya kiuchumi na kisiasa?

Jee! Unafahamu kwamba hakuna kitu kinachoitwa kero za muungano bali muungano wenyewe ndio kero?

Jee! Unadhani ni haki kwa Zanzibar kuwa ni abiria asiye na kauli ndani ya safari ya muungano inayoendeshwa na Tanganyika?

Tafadhali elewa kwamba Zanzibar imekabiliwa na kazi kubwa ya kujinasua kutoka katika utawala wa Tanganyika.

Ikiwa muungano wa Tanzania utaendelea katika muundo wake wa sasa, Zanzibar haiwezi kupiga hatua yeyote mbele. Wakati umefika kwamba ni lazima muungano huo ujadiliwe na kuundwa upya kwa makubaliano yanayoheshimu nchi mbili kwa usawa na haki, laa si hivyo Zanzibar ijitoe katika muungano huo unaodhoofisha mamlaka na uchumi wake.

Katika siku chache zijazo, tunategemea kwamba mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya ya Tanzania utaanzishwa rasmi. Hii ni nafasi adhimu kwa Zanzibar. Ni matarajio yetu kwako ukiwa kama mjumbe wa BLW kwamba utasimama imara kutetea maslahi ya Zanzibar katika suala hili muhimu. Tunaamini kwamba hiyo ni haki ya Wazanzibari kwako ukiwa kama mwakilishi wao.

Mwanzoni mwa Februari mwaka huu, MUWAZA ilitoa tamko juu ya kupatikana kwa katiba mpya ya Tanzania huku ikipendekeza kwamba BLW lipitishe azimio lenye mambo mahsusi ambayo ni lazima yawemo katika katiba mpya ya Tanzania.

MUWAZA inawasilisha kwako kopi ya tamko hilo pamoja na barua hii.

MUWAZA imefarajika kusikia kwamba mjumbe wa BLW, Mh. Ismail Jussa, amekabidhi kwa Mh. Spika hoja binafsi anayokusudia kuiwasilisha katika kikao kinachoendelea kuhusu mjadala wa katiba mpya ya Tanzania. Ingawa hatujui yaliyomo ndani ya hoja hiyo, lakini tunaimani kwamba hiyo ni nafasi nzuri kwa wajumbe wa BLW kuorodhesha yale yote yaliyo muhimu kwa maslahi ya Zanzibar.

Kwa mnasaba huu wa katiba mpya, MUWAZA ingependa ikukumbushe mambo muhimu yafuatayo:

1. Katiba mpya ya Tanzania ni njia pekee ya kuhakikisha kwamba muungano wa Tanzania unajadiliwa upya ili kuufanya uwe wenye maslahi, haki, kueleweka na unaokubalika kwa wananchi wa Zanzibar.

2. Zanzibar inayo haki sawa katika kuijadili katiba mpya ya Tanzania ikiwa mshiriki sawa na Tanganyika. Kwa maana hiyo, miswada yote inayojadiliwa katika Bunge la sasa la Muungano, ni lazima pia ijadiliwe katika BLW.

3. Majadiliano yaanze kwa kuhakikisha kwamba Tanganyika inatoka katika kivuli chake ili Zanzibar ikae na mshirika wake kulijadili suala zima la Muungano.
4. Kwa namna yeyote, suala la katiba mpya lisitumike kama njia ya ujanja ya kuuhalalisha muungano uliopo katika muundo wake wa sasa.

5. Zanzibar iunde Tume huru ya Wazanzibari itakayokusanya mapendekezo ya katiba mpya ya muungano kutoka kwa wananchi wa Zanzibar. Tunapendekeza Tume hiyo ifanye kazi chini ya uongozi wa Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharrif Hamad au Rais Mstaafu Dr. Amani Abeid Karume.

6. Katiba mpya ibadilishe mfumo mzima wa muungano na kuufanya kuwa ni Shirikisho la Tanzania linalojumuisha Zanzibar na Tanganyika. Kwa maana hiyo kuwepo na serikali tatu zenye marais wake kamili – yaani Serikali za Zanzibar, Tanganyika, na Shirikisho la Tanzania.

7. Urais wa Shirikisho uwe wa mtindo wa kupokezana baina ya marais wa Zanzibar na Tanganyika katika kila muhula mmoja wa uongozi. Kwa mfano, katika kipindi cha uongozi cha miaka 5, miaka miwili na nusu iwe kwa Zanzibar na mengine miwili na nusu iwe kwa Tanganyika.

8. Kwa kupitia kura ya maoni, Wazanzibari wawe ndio wenye maamuzi ya mwisho ya kukubali au kukataa muungano, muundo wake mpya, na pia kuikubali au kuikataa katiba mpya.

9. Zanzibar ichukue nafasi ya kuboresha katiba yake ili kuirudishia mamlaka yake yaliyoporomoka kutokana na muungano wa sasa. Katiba ya Zanzibar isiwe ni yenye kutawaliwa na katiba nyengine yoyote.

10.Mamlaka ya mihimili ya Zanzibar ya BLW, SUK, pamoja na Mahakama, yalindwe na yawe ndio ya juu kabisa katika kusimamia maslahi ya Zanzibar ndani na nje ya nchi.

11.Ihakikishwe kwamba maamuzi yanayopitishwa katika Bunge la Muungano la sasa hivi yanazingatia idadi ya thuluthi mbili za wajumbe kutoka kila upande wa muungano.

12.Ihakikishwe kwamba wananchi wanapatiwa elimu ya kutosha kuhusu suala la katiba na kwamba vyombo vyote vya habari vikiwemo vya serikali vinatoa taaluma kwa wananchi kwa ufanisi mkubwa.

MUWAZA inakushukuru na inaamini kwamba utaendelea na jitahada zako za kusimamia maslahi ya Zanzibar kwa uwezo wako wote. Tunakuombea mafanikio.

Naomba kuwasilisha,

Dr. Yussuf Saleh Salim

Mwenyekiti wa MUWAZA

April 5, 2011

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.