Na Halima Abdalla
JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi limeokota bastola moja aina ya ‘Star’ katika eneo la Mkele ambayo ilitupwa na majambazi ambao walikuwa na lengo la kutaka kuiba katika ghala ya pombe lililoko mtaa huo Mjini Zanzibar.
Akizungumza na gazeti hili Ofisini kwake Madema, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Aziz Juma Mohammed, alisema kuokotwa kwa bastola hiyo kunatokana na taarifa kutoka kwa raia wema.
“Taarifa hizo tulizipata kabla ya siku ya tukio hilo kutokea kwamba kunataka kuja majambazi katika eneo hilo usiku wa siku hiyo ya tukio”, alifahamisha Kamanda.
Kamanda alisema kutokana na taarifa hizo walizozipata kutoka kwa msamaria mwema Jeshi la Polisi likaamua kuzifanyia kazi taarifa hizo ambapo siku ya tukio Jeshi la polisi lilifika mapema katika eneo hilo kabla ya majambazi hao kufika na kuamua kusubiria kufika kwao.
Alisema baada ya kufika Jeshi la Polisi baada ya muda walikuja watu watatu na kutuhumu ndio majambazi walioelekezwa na ndipo walipoamua kuwasimamisha lakini walikaidi amri hiyo na kuamua kukimbia.
Alifahamisha kuwa baada ya kukimbia Jeshi la Polisi likafyatua risasi tatu hewani na walitupa kipolo ambacho ndani yake mlikuwa na hiyo bastola, tindo na hook.
Kamanda alisema vitu hivyo vyote vimeshikiliwa na polisi na upelelezi unaendelea kuwatafuta watuhumiwa hao.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kutofumbia macho matukio ya hatari kama hayo yanapotokea na kuwataka kutoa taarifa polisi wanaposikia kunatukio la hatari linataka kutokea katika eneo.
No comments:
Post a Comment