Viongozi wa Wilaya ya Kusini Unguja wametakiwa kuyatatua matatizo yao ya ardhi yanayowakabili ili kuyapatia ufumbuzi na sio matatizo hayo kuyapeleka kwake.
Hayo ameyasema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein wakati wa majumuisho ya ziara yake katika Mkoa wa Kusini Unguja wakati alipokuwa akizungumza na viongozi mbali mbali wa mkoa katika ukumbi wa Chuo kikuu cha Tunguu wilaya ya kati Unguja.
Akizungumza na viongozi wa mkoa huo amesema madiwani, masheha na baadhi ya viongozi wengine ndio chanzo kikuu cha migogoro hiyo ya ardhi.
Dk Shein amesema migogoro ya ardhi inapaswa kutatuliwa na viongozi wa eneo husika na sio migogoro hiyo kupelekwa katika ngazi za juu.
Amesema kuwa maeneo yaliyokumbwa na migogoro hiyo mikubwa ya ardhi ni Mtende na Makunduchi katika Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja.
Akizungumzia juu ya uwajibikaji katika kazi amewataka viongozi wa Mkoa wa Kusini Unguja kutokukaa maofisini bali wawe wanatembelea sehemu mbali mbali za kazi ili kuwafahamisha na kuwaelekeza wananchi juu ya mambo mbali mbali ya utekelezaji wa kazi zao.
Aliwataka viongozi wa majimbo na serikali wasiwe mabahili katika kuchangia maendeleo ya nchi ikiwemo miradi mbali mbali ya maendeleo yaliyopo na yale yatakayoanzishwa
Rais wa Zanzibar Dk Shein amesikitishwa na tabia iliyojitokeza kwa kupelekewa taarifa ya mkoa huo ambayo imeelezea juu ya tatizo mimba za utotoni, uzuwiaji waupigishaji wa disco vijijini na migogoro ya ardhi lakini matatizo hayo hayakujumuishwa katika taarifa ya mkoa wa kusini iliyosomwa na mkuu wa mkoa huo mwanzo wa ziara yake hapo juzi.
Imetolewa na Idara ya habari Maelezo Zanzibar
No comments:
Post a Comment