Kamishna Mkuu wa ZRA Said Kiondo Athumani akitoa hotuba ya Ufunguzi wa Mkutano wa wa 21 wa Kamati ya Uadilifu ya Mamlaka ya Mapato Afrika Mashariki uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Madinatil Bahr Bweni Zanzibar.
MAMLAKA za Mapato Afrika Mashariki zimesisitizwa kuimarisha matumizi ya ushahidi wa kitaalamu (forensic evidence) katika mapambano dhidi ya rushwa na uhalifu wa kifedha ili kulinda mifumo ya mapato na kuimarisha uadilifu wa taasisi za umma.
Kauli hiyo ilitolewa na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Said Kiondo Athumani, wakati akifungua mkutano wa 21 wa Kamati ya Kiufundi ya Uadilifu ya Mamlaka za Mapato Afrika Mashariki uliofanyika katika Hoteli ya Madinat Al Bahr, Mbweni.
Alisema kuimarisha uadilifu ni msingi muhimu wa kuboresha ukusanyaji wa mapato, kulinda uhalali na kuimarisha taswira ya mamlaka za mapato pamoja na nchi kwa ujumla, hasa katika kipindi ambacho nchi za ukanda zinaelekea zaidi katika ujumuishaji wa kiuchumi.
Kamishna Kiondo alieleza kuwa wahalifu wa kifedha na wakwepaji kodi hubuni mbinu mpya kila siku, hali inayohitaji mamlaka za mapato kutumia teknolojia na ushahidi wa kisasa wa kitaalamu ili kukabiliana na uhalifu huo unaovuka mipaka ya kijiografia.
Alibainisha kuwa rushwa katika mamlaka moja huathiri ukanda mzima, kwani mitandao ya kihalifu hutumia mianya iliyopo katika taasisi zilizo dhaifu, hivyo kufanya ushirikiano wa kikanda na ubadilishanaji wa taarifa kuwa jambo la lazima.
Akizungumzia kaulimbiu ya mkutano huo isemayo “Kuimarisha Mapambano Dhidi ya Rushwa Kupitia Ushahidi wa Kitaalamu (Forensic Evidence)”, alisema inalenga kuongeza usahihi wa uchunguzi, kupunguza uingiliaji wa ndani na kuongeza imani ya umma kwa mamlaka za mapato.
Aliwahimiza wajumbe wa mkutano huo kushiriki kwa uwazi, kubadilishana uzoefu, kujadili kesi halisi na kuimarisha matumizi ya teknolojia ya forensics pamoja na kujenga uwezo wa ndani wa uchunguzi katika mamlaka zao.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Abola, alisema nchi wanachama zimekubaliana kuimarisha hatua za kinga, uchambuzi wa hatari za uadilifu na kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma.
Kwa upande wake Katibu wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shaibu Mmari, alisema mamlaka hizo zinaendelea kuimarisha matumizi ya vifaa vya forensics na maabara za kisasa kukabiliana na rushwa na ukiukwaji wa maadili unaofanyika kwa njia za kidijitali.
Mkutano huo wa siku nne uliwakutanisha wajumbe kutoka mamlaka mbalimbali za mapato za Afrika Mashariki, zikiwemo Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Somalia na Zanzibar, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika mapambano dhidi ya rushwa na uhalifu wa kifedha.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uadilifu ya Mamlaka ya Mapato Afrika Mashariki James Abola akitoa hotuba ya makaribisho katika Mkutano wa 21 wa Kamati ya Uadilifu ya Mamlaka ya Mapato Afrika Mashariki uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Madinatil Bahr Bweni Zanzibar.
Meneja Raslimali Watu ZRA Raya Suleiman Abdalla akizungumza katika Mkutano wa wa 21 wa Kamati ya Uadilifu ya Mamlaka ya Mapato Afrika Mashariki uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Madinatil Bahr Bweni Zanzibar.
Mjumbe wa Kamati ya Uadilifu kutoka Nchi ya Somali Ahmed Mohamed Afrah akizungumza katika Mkutano wa wa 21 wa Kamati ya Uadilifu ya Mamlaka ya Mapato Afrika Mashariki uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Madinatil Bahr Bweni Zanzibar.
Kamishna Mkuu wa ZRA Said Kiondo Athumani(KATIKATI)akiwa katika Picha ya Pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Uadilifu ya Mamlaka ya Mapato Afrika Mashariki katika Mkutano wa 21 wa Kamati hio uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Madinatil Bahr Bweni Zanzibar.
PICHA NA YUSSUF SIMAI,MAELEZO ZANZIBAR.17/12/2025.
0 Comments