Habari za Punde

DK SHEIN AHIMIZA UCHUNGUZI WA MACHO KWA WATOTO

Rajab Mkasaba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amezindua Kliniki ya macho katika hospitali ya Chake Chake Pemba na kusisitiza haja ya kuwepo huduma ya kuwafanyia uchunguzi wa macho watoto wachanga mapema wanapozaliwa ili kugundua iwapo wamepata matatizo ya macho.

Dk. Shein aliyasema hayo mara baada ya uzinduzi  wa kliniki hiyo inayofanya kazi ya uchunguzi na utengenezaji miwani katika hospitali ya Chake Chake ukiwa n ushirikiano kati ya ‘Sight Savers’, ‘International Centre for Eye care Education’ (ICEE)  la Afrika Kusini pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ikiwa ni miongoni mwa ziara yake ya kutembelea Mikoa yote ya Zanzibar ambapo, alimalizia ziara yake ya Mkoa wa Kusini Pemba.

Akitoa shukurani zake kwa wahisani Sight Savers pamoja na Shirika la ICEE Dk. Shein alisema kuwa amefurahishwa na hatua za wahisani hao katika kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha huduma za afya kwa jamii.

Dk. Shein alisema kuwa huduma zinzotolewa katika hospitali hiyo ya Chake Chake  ni muhimu kwa wananchi kwani itawasaidia kwa kiasi kikubwa kupata hudma ya  uchunguzi wa macho pamoja na kupata tiba hivyo kuna haja ya  kuanzishwa utaratibu wa kuwapima macho watoto mapema wanapozaliwa ili kujua  iwapo wamepata matatizo ya macho.

Alisema kuwa kutokana na umuhimu huo kuna haja kwa madaktari na wataalamu wa kitengo icho kuanzisha utaratibu huo ambao utasidia kwa kiasi kikubwa kujua afya za watoto wachanga.

Nae Mama Mwanamwema Shein alisisitiza haja ya kuazishwa utaratibu huo ambao utarahisha kwa kiasi kikubwa kugundua matatizo ya macho kwa watoto mara wanapozaliwa.

Alisema kuwa itakuwa si jambo la busara kuja kutibu matatizo hayo ya macho watoto pale wakati matatizo hayo yameshakuwa makubwa na badala yake ni jambo la busara matatizo hayo yakajulikanwa mapema kutokana na kufanywa uhunguzi watoto mara tu wanapozaliwa.

Nae Mkurugenzi Mkaazi wa Sight Savers Dk. Ibrahim Kabole alimueleza Dk. Shein kuwa juhudi zitafanywa katika kuhakikisha utaratibu huo unafanyika kwani tayari wamo katika mchakato ambao wanatarajia kuanza mwezi wa Julai mwaka huu katika kutoa huduma hiyo kwa watoto.

Alisema kuwa tayari Sight Savers wakishirkiana na Shirika la International Centre for Eye Care Education (ICEE) la Durban limeanza kusaidia vifaa kadhaa vya macho.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa kitengo hicho cha upimaji macho ni moja kati ya vitengo viwili ambavyo vimeanzishwa hapa Zanzibar ambapo kimoja kiko katika hospitali ya Mnazi Mmoja Unguja na chengine ndio hicho alichokizindua Rais Shein huko kisiwani Pemba.

Alisema kuwa matengenezo ya chumba hicho cha upimaji na uchongaji wa miwani ulianza mnamo tarehe 2, mwezi wa Februari mwaka huu na kukamilika mwezi wa Machi mwaka huu kwa  gharama za kitanzania Shilingi milioni 3 na kusisitiza kuwa mradi huo unagharimu Shilingi milioni 103.388,100.

Nae Bi Mary Wepo alieleza Dk Shein kuwa ICEE inafanya kazi katika nchi mbali mbali za bara la Asia, Amerika na Afrika ambapo kwa Afrika inafanya kazi katika nchi 11 ambapo lengo lake kubwa ni kukomeza upofu unaoweza kuepukwa kwa kuvaa miwani ifikapomwaka 2020.

Alisema kuwa mnamo mwaka 2009 ICEE pamoja na Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitia saini kwenye MOU huko Dar-es-Salaam ambapo walikubaliana kushirikiana katika uendelezaji wa kukomeza upofu unaoepukika kwa kuvaa miwani.

Wepo alisema kuwa Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea vizuri sana na hadi sasa tayari kumeshaanzishwa kliniki za vitengo vya macho 12 Tanzania Bara na mbili Zanzibar kimoja kikiwa Pemba na chengine Unguja na kufanya idadi ya vituo 14.

Alieleza kuwa kwa muda wa mwaka mmoja wagonjwa 13,148 wamepimwa macho kupitia vituo hivyo na kusisitiza kuwa kuna umuhimu wa kuchukuliwa hatua za makusudi katika kuwawezesha wananchi wa Zanzibar wenye kipato cha chini wasaidiwe ili waweze kununua miwani iwapo wamehakikishia na daktari kutumia miwani.

Mapema akiwa katika hospital hiyo  Dk. Shein alikagua ukarabati wa utanuzi wa maabara ambapo ukarabati huo ulianza Machi 17, mwaka huu na kutarajiwa kumaliza mwanzoni mwa mwezi ujao chini ya msaada wa ICAP.

Mpaka kumalizika kwa ukarabati huo kiasi cha Dola 85,000 zinatarajiwa kutumika ambapo tayari kwa upande wa Wete lab /CTC/ Phamacy  matayarisho yameshaanza ambapo pia, ICAP imekuwa ikitoa mafunzo kwa watoa huduma za afya,kusaidia ajira ya baadhi ya watoa huduma, kusaidia ‘Pemba Public Health Labor’ iweze kufanya uchunguzi wa PCR kwa ajili ya DBS/EID pamoja na ununuzi wa vifaa, madawa ya maabara na upimaja wa Virusi vya Ukimwi.

 Dk Shein kabla ya kutembelea hospitali hiyo alikagua ujenzi wa skuli ya sekondari ya Wilaya iliyopo Wawi pamoja na ujeni wa skuli ya Sekondari ya Wilaya iliyopo Shamiani Chake Chake Pemba na kuwasisitiza wanafunzi waongeze bidii katika masomo yao.

Pia, alikagua ujenzi wa barabara ya Chachamjawiri-Tundauwa, alkagua athari za mazingira na kupata maelezo mafupi huko Vitongoji, alifika katika bonde la mpunga la Mfubaha Vitongoji na kukagua skuli ya wakulima wa muhogo na shamba la kilimo cha mseto yote ya Pujini.

Hapo jana Dk. Shein aliweka jiwe la msingi la nyumba ya Daktari huko Makombeni Wilaya ya Mkoani Pemba na kuwaeleza wananchi kuwa serikali yao itaendelea kuwaunga mkono katika kuimarisha sekta ya afya katika maeneo yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.