Habari za Punde

JIHAD AITAKA SOS KUANZISHA KITUO CHA MICHEZO

Na Ali Amour, WHUUM

SHIRIKA la vijiji vya kulelea watoto yatima SOS, limeshauriwa   kuanzisha kituo cha michezo ili kuibua na kukuza vipaji vya wanamichezo wachanga ambao ni rasilimali kubwa kwa taifa.

Changamoto hiyo imetolewa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Abdilahi Jihad Hassan, katika hafla ya siku ya michezo ya kijiji hicho ikiwa miongoni mwa shamrashamra za kutimia miaka 20 ya kuanzishwa kwake hapa Zanzibar.

Jihad amesema kuwa, hatua iliyofikiwa na SOS katika nyanja za taaluma na michezo ni kubwa, ambapo vipaji vya michezo mbali mbali vimeibuliwa na kuijengea Zanzibar matumaini ya kufanya vizuri katika medani za michezo.

Alifahamisha kuwa, ili taifa liendelee kimichezo, vituo vya kulea vipaji ni la vya lazima, kwani mafanikio ya jambo lolote hutegemea msingi ulio imara.

Waziri huyo ameeleza matumaini aliyonayo juu ya jambo hilo, kwa vile kijiji hicho kina viongozi na wataalamu mahiri katika fani ya  michezo.

Aidha amelipongeza shirika la SOS kwa uamuzi wa busara kuanzisha kijiji cha aina hiyo hapa nchini, na kulitaka liongeze ushirikiano na  mawasiliano ya karibu na wadau wengine wa michezo vikiwemo vyama ili kupata ushauri, maelekezo na hata walimu wa michezo mbali mbali watakayoamua kuianzisha.

Nae Mkurugenzi wa SOS Zanzibar Suleiman Mahmoud Jabir, alimshukuru Waziri Jihad kwa mchango wake mkubwa katika  kukiendeleza kijiji hicho, na kusema kwa upande wao wako tayari kupokea na kuyafanyia kazi maelekezo na ushauri wa kuendeleza michezo nchini.

Katika tamasha hilo, kulifanyika michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na pambano na fainali ya mpira wa miguu baina ya Evarest na Kilimanjaro, ambapo Evarest iliibamiza Kilimanjaro kwa magoli 3 - 1 na kutwaa ubingwa kwa mara ya nne mfululizo.

Maadhimisho ya kutimia miaka 20 tangu kuanzishwa kijiji cha SOS Zanzibar, yanafikia kilele leo Juni 23, 2011.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.