Habari za Punde

PAJE KUHAKIKI WAFANYAKAZI MAHOTELI

Na Mwajuma Juma
KAMATI ya Maendeleo ya kijiji cha Paje wilaya ya Kusini Unguja, leo inatarajia kukutana na wamiliki wa mahoteli kwa lengo la kutaka kujuwa wazururaji na wanaofanyakazi katika hoteli zao.


Kikao hicho ambacho kitafanyika skuli ya Paje kitazungumzia mambo mbali mbali lakini kubwa ni kuwataka wamiliki hao kuwaorodheshea wafanyakazi wao.

Katibu wa kamati hiyo Khamis Seif Ali, alisema kuwa lengo ni kutaka kuwajuwa wafanyakazi na wazururaji ili kuweza kukabiliana na wahalifu wanaoingia kijijini kwao.

Alisema baada ya kumalizika kwa kikao hicho wanakijiji hao wataweza kuingia nyumba kwa nyumba kuwasaka wazururaji na kuwapeleka katika vyombo vya sheria.

“Tunakutana na wamiliki wa mahoteli watuorodheshee wafanyakazi wao na wawapatie vitambulisho baadae tutaingia nyumba kwa nyumba, msitu kwa msitu ili kuwasaka wazurururaji na kwa hili hatutamuonea mtu muhali”, alisema Katibu huyo.

Alisema kipindi hiki cha msimu watu wengi huingia ambao wengine wanakuwa hawana kazi maalumu na badala yake hufanya vitendo vya uhalifu kijijini hapo, hivyo ili kukabiliana na hali hiyo wameona ni vyema wakawaita wamiliki hao kwa kuwaorodheshea wafanyakazi wao.

“Baada ya kikao hicho kutafuatia msako kaamti yao ya ulinzi Shirikishi ili kuwatambua wazururaji”, alisema katibu huyo na kuongeza kuwa hatutomruhusu mtu kuingia katika fukwe zetu tuliyekuwa hatumjui hata kidogo na hali hii itaanza baada ya kikao chetu.

Kijiji cha Paje kina hoteli za kitalii karibu 10 ambapo kamati hiyo ya maendeleo imekuwa na kawaida ya kukutana na wamiliki hao kwa mwaka mara tatu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.