Habari za Punde

SEKTA BINAFSI ZIFANYE KAZI PAMOJA

Na Mwandishi Wetu

MSHAURI wa Bodi ya sekta binafsi kutoka Jumuia ya Afrika Mashariki Lilian Awinja amesikitishwa kutofanya kazi kwa umoja wa sekta binafsi Zanzibar (ABCZ).

Awinja alieleza hayo kwenye warsha ya siku mbili iliyoelezea umuhimu wa umoja wa sekta binafsi katika kukabiliana na matatizo yao mbali mbali ikiwemo ugonjwa wa UKIMWI.


Mshauri huyo alisema ni jambo la kushangaza kuiona ABCZ ikishindwa kufanyakazi zake katika kuwahudumia wananchi Zanzibar sambamba na kushindwa kusimama ipasavyo katika vita dhidi ya maradhi ya UKIMWI.

“Kama ni Wazanzibari ndio walioiunda ni jukumu la sekta hizo kukaa pamoja na kuhakikisha jumuia hiyo inafanyakazi na sio kulalamika”, alisema.

Aidha alisema endapo ABCZ itakuwa ikitekeleza majukumu yake ni rahisi kuuzika kwa miradi yao kwa wafadhili na kupata fedha ambazo zitasaidia kuendesha programu mbali mbali ikiwemo uhamasishaji wa dhidi ya maradhi ya UKIMWI.

“Nyinyi ni watu wa sekta binafsi mmeajiri watu kwa nini msiweke programu za UKIMWI ambazo zitawasaidia wafanyakazi wenu kuepukana na maradhi hayo ambayo yamekuwa tatizo kubwa”.

Aidha mshauri huyo alisisitiza umuhimu wa sekta binafsi kutumia vyombo vya habari katika kuitangaza miradi na mikakati yao ili jamii iweze kufahamu kile wanachokifanya.

Akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi wa Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC), Dk.Omar Makame Shauri alisema suala la UKIMWI ni tatizo linaohitaji kushughulikiwa kwani sio tatizo la kiafya pekee bali ni la kiuchumi, kijamii na kiafya.

Akifungua mkutano huo, Rais wa Jumuia ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima Mbarouk Omar alisema sekta ya utalii pamoja na umuhimu wake lakini inapaswa itazamwe upya ili isiwe kiungo cha ongezeko la UKIMWI.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.