Habari za Punde

BURUDANI ZAOMAN ZATEKA MASHABIKI

Na Aboud Mahmoud

UKUMBI wa Ngome Kongwe Forodhani, juzi usiku uliendelea kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wanaohudhuria maonesho ya utamaduni wa Oman yaliyofunguliwa Julai 13.

Miongoni mwa burudani zlizosisimua na kuwainua mashabiki kila mara kutoka sehemu walizokaa, ni Al-Baraa kutokana na umahiri wa wanenguaji wake jukwaani.

Midundo ya ngoma hiyo, ilisababisha watazamaji waliojazana ukumbini hapo wakiwa mchanganyiko wa wenyeji wa Zanzibar na wa mataifa mengine kupanda jukwaani wakiserebuka kwa furaha.

Wasanii wa ngoma hiyo walivutia hadhira kwa uwezo mkubwa walionesha huku wakishikilia majambia (khanjar), moja kati ya vielelezo vya utamaduni wa Oman.

Kwa kuonesha umuhimu ushirikano wa kiutamaduni kati ya Oman na Zanzibar, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Abdilahi Jihad Hassan, alikuwa tena miongoni mwa wananchi waliohudhuria hafla hiyo kufuatilia kwa kina burudani hizo.

Aidha ngoma ya Lewa nayo ilikuwemo katika orodha ya kazi za sanaa zilizotumbiza ukumbini hapo na kuvuta hisia za wananchi kutokana na ustadi wa wasanii wake kucheza huku wakishikilia fimbo.

Katika ngoma hiyo, kijana wa Zanzibar pia alikaribishwa kucheza na kumudu kuonesha umahiri wa hali ya juu akiwaacha hoi waliohudhuria katika hafla hiyo, huku akinamama wakishindwa kujizuia na kupanda jukwaani kufuatilia midundo maridhawa.

Kwa mujibu wa ratiba ya tamasha hilo, burudani hizo zitaendelea kurindima leo na kufikia tamati kesho, ambapo pia leo kutakuwa na semina katika ukumbi wa Makumbusho ya Kasri Forodhani, ambapo watoa mada kutoka Oman na Zanzibar wataelezea historia ya utamaduni wa nchi hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.