Habari za Punde

KAMISHNA AWAKOMEA WANAOKUMBATIA WAHALIFU

Na Ramadhan Himid Haji.

KAMISHNA wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa amekemea tabia ya baadhi ya wanananchi kuwakumbatia Wahalifu katika maeneo yao wanamoishi hali ambayo inapelekea kuwepo kwa ongezeko la Uhalifu nchini.

  Aliyasema hayo  alipokuwa akizungumza na Kamati za Ulinzi, Usalama na Ustawi wa jamii Shehia za Koani na Ubago Wilaya ya Kati Unguja katika mfululizo wa ziara zake za kutembelea  shehia za Mkoa wa Kusini Unguja katika kuandaa mikakati imara juu ya  kukabiliana na changamoto mbali mbali za Uhalifu.

     Alisema kwa ujumla takwimu za Uhalifu zinaonyesha kushuka kwa kiwango kikubwa lakini kuna baadhi ya maeneo hali sio nzuri kwa vile bado wananchi wake hawajaamua kuanzisha Kamati za Ulinzi na Usalama kwa minaajili ya kukabiliana na viotendo vya kihalifu.

     Alitolea mfano wa makosa ya Uvunjaji kwa miezi sita kutoka Januari hadi Juni, 2011 Mkoa wa Kusini Unguja una jumla ya makosa 56 na kati ya hao mengi yao yameripotiwa maeneo ya Koani, Kianga na Mwera.

   “ Napenda nikuambieni wananchi wa Koani na Ubago kwanini hivi sasa Uhalifu Mjini umepungua na kwenu umezidi ni kutokana na ukweli kwamba hamjaimarisha Kamati zenu za Ulinzi na Usalama na kwasababu hiyo Wahalifu wa Mjini wamehamia maeneo yenu, mnahitaji kujipanga kweli kwani dhana ya Ulinzi Shirikishi inagusa kila mwanajamii kwa nafasi yake…..”, alisema Kamishna. 

    Alisema Kamati za Ulinzi na Ustawi wa jamii ni injini muhimu ya kuzaa fikra na maarifa mapya ya kutatua kero za Uhalifu kwani zipo Shehia ambazo zilikuwa na matatizo sugu ya kihalifu lakini baada ya kuanzishwa kwa Kamati hizo Uhalifu umepungua.

    Alibainisha kwamba iwapo Kamati hizo zitafanya vikao mara kwa mara, kupeana taarifa na kuzipatia ufumbuzi taarifa hizo, vitendo vya kihalifu vinaweza kutoweka lakini kama wataendelea kuoneana muhali miongoni mwao watajikuta wakiishi katika hali ya wasi wasi.

     Mapema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi wa Polisi Augustino Olomi amewaambia wananchi wa Koani na Ubago kuwa Polisi Jamii ikitekelezwa kwa vitendo ndio jibu sahihi juu ya kilio cha kero zao katika maeneo yao wanayoishi.

    Nao Wananchi wa Koani na Ubago wamemuomba Kamishna wa Polisi kudumisha mashirikiano na wananchi kwani Shehia zao mbili zina wimbi kubwa la wizi wa mazao kiasi kwamba wakulima wengi wana hali ngumu ya kimaisha kutokana na kushamiri kwa wizi wa mazao yao.

  “Ndugu Kamishna wananchi wa Shehia hizi mbili tuna kilio kikubwa, hatuvuni mazao yetu yakipea hata siku moja na tukisubiri yapee wanatokea wajanja wa kuyavuna kabla ya kuvuna sisi wenyewe, tusaidie kwa hili mheshimiwa tuna hali mbali”, alisema Bw. Makoe Shaaban.

   Ziara hizo za Kamishna wa Polisi Zanzibar , Mussa Ali Mussa ni miongoni mwa mikakati yake ya kueneza Sera ya Polisi Jamii/Ulinzi Shirikishi ambapo tayari ameshazitembelea Shehia 74 za Mkoa wa Mjini Magharibi na hivi sasa yumo katika ziara yake Mkoa wa Kusini Unguja.
   

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.