Vigogo wadaiwa kufumbia macho amri za mahakama
Na Aboud Mahmoud
WAKATI Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein akiwaagiza viongozi kuondosha tatizo la migogoro ya ardhi kwa wananchi, bado baadhi ya wananchi wanalalamikia kuchukuliwa kwa nguvu maeneo yao.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa masikitiko watoto wa wamiliki wa eneo moja huko Shakani Unguja wamesema eneo hilo linamilikiwa na koo mbili ya Said Iddi Bavuai na Abdallah Ahmed tangu
mwaka 1920.
Walisema kuwa eneo hilo lenye heka 300 hadi 400 limekuwa na matatizo kwa muda mrefu sasa ambapo walieleza kuwa wameshapandishwa mahakamani zaidi ya mara tano ambapo mara zote wamekuwa wakishinda kesi lakini kinachowashangaza kwamba kwamba haki yao inaendelea kung'ng'aniwa wale waliowaita vigogo.
"Shamba hili ni mali yetu tumerithi kwa wazee wetu ambapo hivi sasa wote wamefariki na amebakia mzee wetu mmoja Abdallah Ahmed na tumefikishana mahakamani mara nyingi na zote tunashinda tunaambiwa hii ni haki ya familia hizi mbili, lakini kinachotushangaza bado eneo hili linachukuliwa na vigogo wa nchi hii,"alisema Alawi Abdallah Ahmed.
Alifahamisha kuwa mgogoro huo umechukua muda mrefu na kwa mara ya kwanza ilitolewa hukumu na walalamikaji wakashinda, hukumu ambayo ilitolewa hukumu na Kadhi wa Mahakama ya Wilaya, Marehemu Yussuf Abdulrahman kati ya mwaka 1973-74.
Walisema baadae iliendelea kwa Kadhi Mkuu wa Zanzibar, marehemu Sheikh Ameir Tajo na pia walishinda,lakini iliweza kwenda mbele zaidi hadi kwa hakimu wa Mahakama kuu ya Zanzibar mwaka 1978 chini ya Jaji Agostino Ramadhan.
Wamiliki hao walisema kuwa mbali na hakimu huyo pia kesi hiyo ilifikishwa kwa hakimu Nassor Mzava, Hamid Mahmoud, Mshibe Ali Bakari ambapo mwisho ilimalizia kwa Jaji Abraham Mwampashi ambae alisema kuwa ardhi hiyo ni mali ya koo mbili hizo.
"Nashangaa kila tunapokwenda tunashinda lakini bado watu wanajichukulia wengine wanawatishia watu tuliowauzia kuwa watawavunjia nyumba zao na pia wao wenyewe kujichukulia viwanja na kujenga,"alisema
Iddi Mohammed Bavuai.
Iddi Bavuai alifahamisha kuwa sehemu ya eneo lilichukuliwa na Ofisi ya Waziri Kiongozi na kupewa uongozi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Baharini ambapo walishindwa kujenga na baadae likachukuliwa na mtu
aliemtaja kwa sasa ni marehemu Suleiman Yahya na baadae walikuja wachina na kuanza kuweka mabati kwa ajili ya ujenzi nao pia waliondoka.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkurugenzi wa Idara ya Ardhi na Usajili,Januari Fussi amekiri kuwepo kwa mgogoro huo na kutaka maamuzi ya vyombo vya juu vya sheria yaheshimiwe.
Alisema kwa sababu vyombo vya juu vya sheria vimeshatoa hukumu ni lazima viheshimiwe.vyuwa kutokana na mgogoro huo kuwa umeshatolewa maamuzi ya kisheria na mahakama hakuna budi kutekelezwa masharti hayo na kuwaachia wamiliki wa ardhi hiyo kuwa mali yao.
No comments:
Post a Comment