Habari za Punde

ZANZIBAR YATANGAZA MIKAKATI MAPINDUZI YA KILIMO

·       Yawasilisha bajeti kumuinua mkulima·       Yashusha bei pembejeo asilimia 50
·       Mbegu bei chini, huduma za kilimo bei chee

Na Mwantanga Ame

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetangaza dhamira yake ya kupunguza bei za pembejeo za kilimo pamoja na kuwapatia ruzuku wakulima.


Hatua hii ya serikali inakuja ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein katika kuelekea Mapinduzi ya kilimo Zanzibar.

Waziri wa Kilimo na Maliasili, Mansoor Yussuf Himid, aliyasema hayo jana wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2011/2011, katika kikao kinachoendelea cha Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Mansoor, alisema serikali imeamua kutekeleza hilo ikiwa ni hatua ya dhamira yake ya dhati ya kuwasaidia wananchi kukabiliana na  tatizo la umasikini, ambapo itatekeleza utoaji wa ruzuku pamoja na kurasimisha utaratibu wa utoaji wa ruzuku ili uwe sehemu ya sera na mipango ya serikali.

Aidha alisema kuanzia sasa bei ya mbolea aina ya TSP kwa kilo itauzwa kwa shilingi 300 kutoka shilingi 600 huku polo moja litakuwa ni shilingi15,000 kutoka shilingi 30,000 ambapo serikali itagharamia kwa polo shilingi 60,000 ikiwa sawa na asilimia 75.

Akiendelea Waziri huyo alisema, bei ya mbolea aina ya Urea bei mpya itauzwa kwa shilingi 200 kutoka shilingi 400 ambapo kwa polo litauzwa shilingi 10,000 badala ya bei ya zamani ya shilingi 20,000 na serikali itagharamia shilingi 40,000 ikiwa sawa na asilimia 75.

Kuhusu bei ya mbegu ya mpunga Waziri huyo alisema, bei mpya itauzwa kwa shilingi 200 kutoka shilingi 500 ambapo kwa polo litauzwa shilingi 10,000 badala ya bei ya zamani ya shilingi 25,000 na serikali itagharamia shilingi 60,000 ikiwa sawa na asilimia 83.

Huduma za matrekta Waziri huyo alisema nazo zimepunguzwa ambapo mkulima ataehitaji kuchimbiwa kwa eka atalipa shilingi 16,000 badala ya shilingi 32,000 ambapo gharama halisi kwa heka ni shilingi 64,000 ikiwa ni sawa na asilimia 75.

Gharama za kuburuga alisema mkulima kwa eka atalipa shilingi 16,000 badala ya shilingi 32,000 ambapo gharama halisi kwa heka ni shilingi 64,000 ikiwa ni sawa na asilimia 75.

Dawa ya magugu alisema itauzwa kwa shilingi 6,000 kwa lita badala ya shilingi 12,500 ambapo gharama halisi ambazo serikali imeamua kuzibeba ni shilingi 12,500 ikiwa ni sawa na asilimia 52.

Aidha, Waziri huyo katika kutekeleza programu ya uimarishaji miundombinu ya masoko, uongezaji wa thamani ya mazao na huduma za fedha vijijini, serikali inakusudia kuzijenga barabara zote ziingiazo mashambani ambazo zitaunganishwa na barabra kuu ikiwa ni hatua itayosaidia kuyafikia masoko kwa urahisi.

Eneo jengine ambalo wanakusudia kulifanyia kazi ni ujenzi wa masoko ya Wilayani yatayokuwa na huduma za uhifadhi wa bidhaa zinazoharibika, na ujenzi wa viwanda viwili vya kuzalisha barafu ambapo kimoja kitakuwa Unguja na chengine ni kwa Pemba.

Alieleza kuwa mradi huo ambao serikali utautekeleza kupitia mkopo uliopewa Tanzania kutoka katika mfuko wa kimataifa wa mendeleo ya Kilimo (IFAD) wa dola za kimarekani 90.6 milioni, utashirikisha pamoja na kuimarisha vikundi vya wajasiriamali katika usindikaji na usarifu wa bidhaa za kilimo.

Alisema kuwa mradi huo pia utahusisha utoaji wa mafunzo ya usanifu na usindikaji bidhaa za kilimo kwa wakulima wajasiria mali na watoaji wa huduma, kuanzisha huduma za utoaji wa fedha kwa wakulima vijijini na kutayarisha  sera ya upatikanaji wa huduma za fedha kwa wakulima na wajasiriamali wadogo wadogo.

Waziri huyo pia alieleza eneo jengine ambalo serikali italiangalia kupitia mradi huo litahusu uanzishwaji kuziwezesha taasisi za kijamii za utoaji wa huduma za fedha vijijini.

Kuhusu zana za kilimo, alisema wanakusudia kuagiza matrekta mapya makubwa manane, matrekta madogo 16 majembe ya kulimia 24 majembe ya kuburugia 24, power tillers 50 seed drillers 50, mini combine harvesters 3, rice reapers 30 na threshers 30.

Zana hizo alisema zitarahisisha kazi za matayarisho ya ardhi ili kuwawezesha wakulima kuwahi msimu wa kilimo na kupunguza upotevu wa mpunga kabla ya baada ya mavuno ikiwa pamoja na kuvutia vijana kufanya kazi za kilimo.

Kuhusu kuwadhibiti nzi wa matunda, alisema Wizara hiyo inakusudia kusambaza mitego 43,000 itayoweza kunasa nzi dume wa matunda kwa kuzikamilishia wilaya za Mkoani Pemba na Kaskazini kwa Unguja.

Kuhusu hali ya lishe kwa wananchi wa Zanzibar, Mansoor alisema si nzuri na hivi sasa Wizara hiyo inakusudia kuwasilisha maombi ya mradi wa lishe unaotarajiwa kutekelezwa chini ya programu ya lishe inayofadhilia na serikali ya Marekani na Ireland kupitia mpango mkuu wa ‘Feed the Future’.

Kuhusu kilimo cha umwagiliaji Waziri huyo alisema kwa mwaka ujao wa fedha Wizara hiyo alisema tayari baadhi ya mambo ya msingi yameweza kufanyika katika kuimarisha mabonde ya kilimo kwa kuwekewa miundombinu ya umeme na hivi sasa wanajipanga kuona kilimo hicho kinaendelezwa.

Alisema Wizara hiyo inakusudia kusambaza na kuzalisha tani 140 za aina mpya ya mbegu bora za juu  NERICA na tani 215 ya mbegu ya mabondeni ili kuongeza utumiaji wa mbegu bora kutoka asilimia 0 kwa kilimo cha juu hadi kufikia asilimia 10 na kutoka asilimia 19.4 hadi asilimia 33.6 kwa kilimo cha mabondeni.

Ili kufanikisha malengo hayo Waziri huyo, aliliomba baraza hilo kumuidhinishia shilingi 15,306,631,000 kwa mwaka wa fedha 2011/2012, ambapo kati ya fedha hizo shilingi 6,623,000,000 kwa ajili ya kazi za kawaida na shilingi 500,000,000 ni ruzuku kwa ajili ya Chuo cha Kilimo Kizimbani na shilingi 8,183,631,000.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.