Habari za Punde

SPIKA KIFICHO: 'BACK BENCHERS' NI KIBOKO


Asema wanawachangamshwa mawaziri
Dk. Migoro UN imefurahishwa hali ya Zanzibar

Na Himid Choko, BLW                      

SPIKA Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Pandu  Ameir Kificho amesema  wajumbe wa Baraza hilo hasa wale wasiokuwa mawaziri (Back  Benchers),  wamekuwa makini zaidi kufutilia utendaji wa serikali jambo ambalo ni  wajibu wao wa kikatiba.


Alisema hatua hiyo imekuwa ikileta changamoto kwa mawaziri na serikali kwa ujumla na kuongeza uwajibikaji, ambapo mawaziri wasipokuwa makini wanaweza kujikuta wajumbe wanaelewa zaidi kuhusiana na wizara zao kuliko wao wenyewe.

Spika Kificho alisema jana wakati akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dk. Asha Rose Migiro huko ofisini kwake Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Alisema katika mkutano wa bajeti uliomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita mijadala ya mkutano huo ilikuwa kivutio na kutoa msisimko mkubwa  kwa wananchi kutokana na umakini wa wajumbe wa Baraza hilo kuhoji na mawaziri kujibu hoja mbali mbali.

“Ingawa hivi sasa hakuna kambi ya upinzani, lakini Baraza limekuwa likiendelea vizuri na kuwavutia wananchi wengi kwani ‘Benchers’ wamekuwa makini kuhakikisha utendaji unakwenda vizuri chini ya usimamizi wa Baraza la Wawakilishi”, Kificho alimueleza Dk. Migiro.

Naye Naibu Dk. Migiro alisema Umoja wa Mataifa umefurahishwa na hatua iliyofikiwa na Zanzibar  kwa kiungia katika mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na mafanikio  makubwa yaliyofikiwa na kuwa mfano wa kuigwa duniani.

Alisema Umoja wa Mataifa unaamini kwamba mfumo huo umechangia kwa kiasi kikubwa hali ya amani na utulivu uliopo hapa nchini.

Alisema hali ya mambo Zanzibar imekuwa kivutio kikubwa kwa Umoja huo katika kutoa fursa nzuri zaidi ya kusaidia nyanja mbali mbali za maendeleo hapa Zanzibar.

“Amani na utulivu ni miongoni mwa mihimili mikuu ya Umoja wa Mataifa , tutapokuwa na amani kwenye nchi ndipo na sisi Umoja wa Mataifa tunapokuwa na fursa nzuri zaidi ya kusaidia kufikia katika maendeleo”,  alisisitiza Dk. Migiro  ambae alikuwa  akitoa salamu za Katibu Mkuu wake , Ban Kimoon.

Alisema umoja huo  unafuatilia kwa karibu utendaji wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya muundo wa Umoja wa Kitaifa na umeridhishwa na utendaji wa serikali hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.