Mwanajuma Abdi, Xiamen China
SHIRIKA la Uwekezaji Vitega Uchumi la Xiamen (Xiamen Investment Promotion Agency) la China, limesema limefungua milango ya uwekezaji kutoka nje na ndani ya nchi, ambayo imesaidia kukuza uchumi na kuongeza pato la taifa kwa haraka.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Manispaa ya Xiamen, Fu Rurong alieleza hayo alipokuwa akitoa taarifa kwa ujumbe wa maofisa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ulioongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame walipofika katika Ofisi hiyo, iliyopo Manispaa ya Xiamen China.
Alisema mafanikio ya ukuaji wa uchumi yameongezeka kutokana na kufungua milango ya uwekezaji kwenye maeneo maalum yaliyotengwa, hali iliyochangia kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa mbali mbali zikiwemo za vifaa vya umeme.
Alieleza serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia mji wake wa Xiamen uliamua kwa makusudi kukaribisha mashirika na makampuni ya uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi katika nyanja tofauti kwa lengo la kukuza uchumi, sambamba na kutoa ushirikiano wa kutosha katika uzalishaji wa bidhaa zikiwemo za teknolojia ya mawasiliano na utengenezaji wa magari.
Alisema katika eneo hilo ipo kampuni maarufu ya kutengeneza magari duniani ya Japani, TOKOYO, huku makampuni ya Taiwani yamefungishwa mkataba katika kukuza masoko ya kibiashara.
Alifafanua kuwa pato la uchumi la taifa limeongezeka kutoka mwaka 2006 hadi 2010 kwa kufikia dola za Marekani bilioni 2053.7, hali ambayo imeongeza pato la wananchi wa kawaida.
Aidha alifahamisha kuwa, Xiamen imekuwa na ongezeko kubwa la watalii kutokana kupakana na nchi mbali mbali za karibu, jambo ambalo limesaidia wananchi kutoka maeneo kadhaa ya dunia kutembelea mji huo wenye vivutio vya kitalii pamoja na kununua bidhaa zinazozalishwa hapo.
Mapema Makamu Meya wa Manispaa Xiamen, Huang Ling alisema Zanzibar ina nafasi kubwa ya kukuza uchumi kupitia katika maeneo tengefu ya uchumi hasa ikizingatiwa visiwa hivyo vinapokea idadi kubwa ya watalii.
Alishauri kuijengea uwezo Manispaa ya Zanzibar ili iweze kufanyakazi kwa ufanisi na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato kwa ajili ya kukuza huduma katika mji.
Alisema Manispaa ya Xiamen imekuwa ikikusanya mapato kutoka katika vyanzo mbali mbali vya jiji hilo, ambazo zinasaidia kuimarisha huduma mbali mbali za kijamii, kiuchumi na kuuweka mji katika usafi, ambapo pamoja na ukusanyaji huo lakini serikali kuu pia inawaongeza fedha za kumudu kuendesha shughuli hizo.
Alifahamisha kuwa, shughuli za kuimarisha uchumi licha ya kutegemea serikali kuu, lakini nao wanachangia kwa kiasi kikubwa ili kupiga hatua za haraka za maendeleo.
Kwa upande wake Dk. Mwinyihaji Makame, alisema Xiamen imepiga hatua kubwa katika usafi wa mji pamoja na maendeleo kwa ujumla, na kubainisha kuwa wakati umefika kwa Zanzibar kuweza kutatua kasoro zinazowakabili ikiwemo nidhamu za kuweka mji safi na watu waachane na tabia ya kutupa taka ovyo.
Alifahamisha kuwa, suala la uimarishaji wa miundombinu ya barabara, bandari, uwanja wa ndege pamoja na huduma za kijamii kama maji, Xiamen wamefanikiwa, ambapo hali hiyo imechangia kuongezeka kwa kasi ya kukua uchumi hali ambayo pia imechangiwa na uwekezaji wa miradi mbali mbali.
Nae Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Abdilahi Jihadi Hassan akitoa shukurani kwa niaba ya ujumbe huo, alisema Zanzibar imepata nafasi kubwa ya kujifunza masuala mbali mbali katika kuhakikisha uchumi wake unakuwa kwa kasi, ikiwa pamoja na kukuza miundombinu ya barabara, uwanja wa ndege na bandari kwa vile nchi hiyo ni visiwa hivyo watu wanategemea usafiri katika shughuli za kijamii na kimaendeleo.
Mimi naomba nichangie kidogo kuhusu hiyo nidhamu ya kuweka mji safi anayoisema waziri,uchafu sio taka peke yake, ni pamoja na vinyesi mikojo n.k. jee anajua kua mji wa z'bar hadi hii leo hauna public toilets za kutosha? ukitoa zile za stand ya darajani na zile za forodhani walizojenga wakoloni? hata maduka yakijengwa hayajengwi na vyoo watu wanategemea chochoro,kuta za nyumba na misikiti ambayo haiko wazi muda wote.hebu tutunge sheria ndogo ndogo kuadhibu wanao jisaidia au kutupa taka ovyo, na kama hatuwezi kujenga vyoo tutangaze tenda ni biashara hiyo!Tusiwe tunasifia watu tuu,na kwetu inawezekana!
ReplyDelete