Habari za Punde

KIKAO CHA BARAZA KIMEANZA LEO

Na Khamis Amani

MKUTANO wa tano wa Baraza la nane la Wawakilishi la Zanzibar, unatarajiwa kuanza Oktoba 12 mwaka huu.

Mkutano huo wa wiki mbili, utafanyika kati ukumbi wa Baraza hilo ulioko Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar na kuhusisha mambo mbali mbali.


Kwa mujibu wa Katibu wa Baraza hilo Ibrahim Mzee Ibrahim, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Barazani hapo alisema, miongoni mwa mambo yatakayojitokeza katika kikao hicho ni uwasilishwaji wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali Zanzibar kwa mwaka 2009/2010.

Ripoti nyengine itakayowasilishwa ni ya ukaguzi yakinifu wa udhibiti na uhifadhi wa mali za kudumu za serikali, pamoja na ripoti ya ukaguzi yakinifu wa miradi ya maendeleo ya wananchi na miradi ya TASAF.

Ripoti hiyo itawasilishwa na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haji Omar Kheri na baadae kuwasilishwa katika Kamati ya PAC kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Kwa upande wa serikali, Katibu huyo alisema kuwa kutawasilishwa sheria ya kuweka masharti ya kuanzisha maabara ya Mkemia Mkuu wa serikali pamoja na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Alifahamisha kuwa, muswada huo utawasilishwa Barazani hapo na Waziri wa Afya Juma Duni Haji.

Mswada mwengine wa sheria unaotarajiwa kuwasilishwa ni wa kuanzisha Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC), pamoja na kuweka masharti bora kwa ajili ya usarifu, uendelezaji, uzalishaji biashara na ukuzaji karafuu na mazao mengine ya kilimo pamoja na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Alisema kuwa muswada huo utawasilishwa na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Nassor kwa ajili ya kupatiwa baraka na wajumbe wa mkutano huo.

Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Othman Massoud anatarajiwa kuwasilisha mswada wa sheria kwa kurekebisha baadhi ya sheria mbili na kuweka masharti bora ndani yake.

Mswada huo ni kufuta sheria ya ulipaji mafao ya viongozi wa Kitaifa namba 4/1988 na sheria ya viongozi wa Kisiasa namba 6/1999 na kutunga sheria mpya ya kustaafu pamoja na mambo mengine yanayohusiana nayo.

Aidha katika kikao hicho, wajumbe kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) watapata nafasi ya kumchagua mjumbe mmoja mwanamme, kwa ajili ya kuwakilisha Baraza hilo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nafasi hiyo inafuatia baada ya kuachwa wazi kutokana na kifo cha Mussa Khamis Silima aliyekuwa akiishikilia.

Kwa mujibu wa Katibu huyo, kabla ya shughuli hizo kufanyika kama kawaida yake mkutano huo utafuatiwa na kipindi cha maswali na majibu, ambapo Mawaziri watapata nafasi ya kujibu maswali mbali mbali watakayoulizwa na wajumbe wa mkutano huo.

Jumla ya mswali 96 hadi hivi sasa yanatarajiwa kuulizwa katika mkutano huo tano unaotarajiwa kuanza majira ya saa 3:00 za asubuhi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.