Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amekitaka kikosi maalum cha kuzuia magendo ya karafuu cha Msuka, Mkoa wa Kaskazini Pemba kufanya kazi kwa mashirikiano zaidi ili kuhakikisha zao la Karafuu msimu huu halitoroshwi nje ya nchi kwa njia ya magendo.
Maalim Seif ameeleza hayo leo huko Msuka alipokuwa akiendelea na ziara yake yakutembelea na kujionea shughuli mbali mbali za ununuzi wa zao hilo katika vituo ikiwa ni mfululizo wa ziara yake ya siku nne kisiwani Pemba.
Amesema zao la karafuu ni zao tegemezi kwa uchumi wa Zanzibar hivyo iwapo wajanja wachache watawaruhusu kulisafirisha zao hilo kwa njia ya magendo itakuwa ni hasara kubwa kwa taifa katika kuendeleza uchumi wake.
Hivyo amekisisitiza kikosi hicho kuhakikisha kuwa kinatekeleza wajibu wake ili kuhakikisha zao la karafuu msimu huu halitoroshwi hata kilo moja kwa njia ya magendo.
Amefahamisha kwamba msimu wa uchumaji uliopiata inadaiwa baadhi ya Askari wa vikosi vya SMZ wasiokuwa waaminifu wakishirikiana na raia katika kulitorosha zao hilo hivyo ametahadharisha kuwa msimu huu serikali iko macho na haitomvumilia mtu yeyote atakaebainika kujishirikisha na vitendo hivyo.
Mapema Makamu huyo wa kwanza ameipongeza hatua ya wananchi kwa kujitokeza kuuza kwa wingi karafuu zao katika vituo mbali mbali vya ununuzi wa karafuu.
Vituo alivyovitembelea ni pamoja na kituo cha Finya, Chonga ,Wambaa,Mtambile na kikosi maalum chakuzuia magendo kilichoko Msuka Pemba.
No comments:
Post a Comment