Habari za Punde

MISAADA MAAFA YA MV SPICE YAZIDI KUMIMINIKA


Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe Ali Nassor akimkabidhi Mwenyekiti wa Kamati ya maafa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mchango wa mkoa wa Lindi kusaidia mfuko wa maafa wa Zanzibar kufuatia kuzama kwa meli ya Mv Spice hivi karibuni

Jamii ya Watanzania itaendelea kukumbuka janga la kuzama kwa Meli ya M.V Spice Islanders lililopelekea kuleta maafa yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa.

Kauli hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mh. Ali Nassor, Mjumbe wa Umoja wa Madereva wa Tax Zanzibar Bw. Chimbeni Kheir pamoja na Mwakilishi wa Baraza la Misikiti Tanzania { Bamita } Mkoa wa Pwani wakati wakizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.



Wawakilishi hao ambao walikuwa wakitoa salamu zao za pole kwa Balozi Seif kufuatia Ajali ya Meli ya M.V Spice Islanders wamesema Msiba uliotokea wa ajali hiyo utabakia kuwa Historia katika Majanga yaliyowahi kuikumba Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema suala la kufarijiana miongoni mwa jamii wakati wanapopatwa na msiba ni utamaduni wa Kiafrika.

Balozi Seif amesema anafarajika kuona kuwa bado jamii nzima nchini inaendelea kuguswa na Janga hilo ambalo limemuathiri kila mwananchi.

Michango aliyokabidhiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi inatoka kwa Uongozi wa Mkoa wa Lindi , Umoja wa Madereva wa Texi Hapa Zanzibar pamoja na Baraza la Misikiti Tanzania { Bamita } Mkoa wa Pwani.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.