Habari za Punde

WANANCHI IJADILINI ADHABU YA KIFO - BALOZI SEIF

Na Faki Mjaka-Maelezo

Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Idd amewataka wananchi wa Zanzibar kwa pamoja waijadili Sheria ya adhabu ya kifo na kudai kuwa si jambo la busara kuachiwa wasomi peke yao kujadili sheria hiyo.

Amesema wananchi wa Zanzibar kwa umoja wao wanapaswa kuijadili sheria hiyo kama inafaa au haifai na si vyema wasomi wakaachiwa peke yao kuijadili sheria hiyo ambayo utekelezaji wake umekuwa mgumu kufanyika katika mataifa mengi.


Balozi Idd ameyasema hayo leo katika maadhimisho ya kuunga mkono tamko la Umoja wa Mataifa juu ya adhabu ya kifo duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Eacrotanal mjini Zanzibar.

Amesema adhabu ya kifo ambayo imehalalishwa katika vitabu vitakatifu vya Kuran na Agano la Kale imekuwa ikipata changamoto nyingi kutokana na ugumu wa utekelezwaji wake jambo ambalo hupelekea wanaharakati wengi kupinga uhalali wake.

Aidha amewataka wasomi wa Zanzibar wenye uwezo wa kuandika kuendelea kuandika vitabu na machapisho mbali mbali yanayohusu Zanzibar jambo ambalo litaipandisha hadhi Zanzibar.

Amesema si vyema kwa mambo ambayo yanatokea katika ardhi ya Zanzibar kuandikiwa na wasomi kutoka nje ya Zanzibar jambo ambalo hupelekea kasoro nyingi za ushahidi.

Maadhimisho hayo pia yalitoa fursa kwa Balozi Seif kuzindua rasmi vitabu viwili ambavyo vipo chini ya udhamini wa kituo cha huduma za sheria Zanzibar.

Vitabu vilivyozinduliwa ni pamoja na “Adhabu ya Kifo katika Sheria za Kiislamu” kilichotungwa na Dk. Muhyiddin Ahmad Khamis na “Zanzibar the Development of the Constitution” ambacho kimehaririwa na Prof. Chris Maina.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa pia Viongozi mbalimbali wa kiserikali akiwemo Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Abuubakar Khamis, Wanasheria, Mawakili, mashekhe na wadau mbalimbali wa Zanzibar.

2 comments:

  1. Asalamu alaykum

    Kwa kweli nampongeza mheshimiwa makamo, issue hapa ni kuangalia kwa kina zaidi kwani wasomi wengi huwa hawaangalii mantiki na mazingira ya sehemu husika wanapojadili vitu ambavyo Dunia ina kampeni maalum.
    Kwenye hili dunia inayo kampeni maalum ya kuondowa adhabu ya kifo, ila sisi wazanzibari tunatakiwa tuwe makini na hilo.
    Mimi nahisi kuhusu hazi kampeni za kilimwengu tusiburutwe kama vile akili zetu haziwezi kufikiria.
    Nnavoelewa huwa tunaiga baadhi ya mambo kwa kuona mafanikio yake sehemu ambazo jambo hilo limekuwa practice, kwa mfano nimeshangaa sana kuona serikali imeiga eti, watoto wasichapwe mashuleni wakati tumeona nchi nyingi za ulaya matokeo ya sheria kama hizi ni kuchipuka watoto wasiokuwa na adabu na ushuhuda ni yale yaliyotokea uingereza hivi karibuni.
    Nikirudi kwenye adhabu ya kifo, karibuni huko nyumbani kulifanyika kongamano la kuhusu madawa ya kulevya, na mmoja kati ya washiriki kutoka Singapore, alisema kuwa katika mambo ambayo yamechangia kutokomeza tatizo la madawa ya kulevya nchini kwake ni Uzalendo na maadii ya Wahusika lakini kikubwa zaidi ni ADHABU YA KIFO.
    Sasa jee tuangalieni marekani, Uingereza na sehemu nyengine zilizokuwa hazina adhabu ya kifo, na nchi kama Singapore ambazo zina adhabu ya kifo katika suali hili ni ipi imefanikiwa.

    Mimi kwa maoni yangu ni kuwa hii sheria ibaki na then tuongeze katika baadhi ya mambo kama madawa ya kulevya na kubaka yawemo katika adhabu hii.

    ReplyDelete
  2. Tatizo hapa si kuiga bali kushindwa kujipanga na badala yake kutegemea sana misaada ya watu!..mwishoe haya mambo tutalazimisha hasaa!Mimi nashangaa.. viongozi wakataa hata kusaini hukumu za watu waliokwisha hukumiwa vifo kwa kuuwa wenzao!..kazi..kweli kweli!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.