Na Ali Bakar
IKIWA ndio kwanza ligi daraja la kwanza taifa imeingia raundi ya tatu, waamuzi wanaochezesha ligi hiyo, wameanza kuzua wasiwasi wakidaiwa kushindwa kuzitafsiri sheria na kuonesha mapenzi kwa baadhi ya timu na kuzihujumu nyengine.
Barua za malalamiko dhidi ya waamuzi hao, zimeendelea kupiga hodi katika ofisi ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kikitakiwa kuwanyoosha waamuzi kama hao kwa kuwachukulia hatua za kinidhamu.
Malalamiko ya hivi karibuni, yametoka kwa timu ya Kijichi Stars iliyomshtaki muamuzi Ramadhan Ibada Kibo, kwa madai kwamba aliikandamiza timu hiyo ilipocheza na Mtende Rangers Oktoba 19, katika mchezo wa ligi hiyo.
Katika pambano hilo lililochezwa kwenye uwanja wa Dimani ambapo Mtende Rangers ilishinda kwa bao 1-0, uongozi wa Kijichi ulimshushia lawama Kibo, ukisema kwa makusudi muamuzi huyo alizopinda sheria, na kuinyima haki timu hiyo na hivyo kuifanya ipoteze mchezo huo.
Ulitoa mfano kwa kusema katika dakika ya pili ya mchezo, beki mmoja wa Mtende alimrejeshea mpira mlinda mlango wake, naye alipoucheza kwa mguu na kumpita huku ukielekea nyavuni, alijaribu kuukamata kwa mikono na kuupiga nje, na muamuzi kushindwa kuamua goli au adhabu.
“Lakini kwa mshangao, muamuzi aliamua mpira huo urushwe badala ya kuwa goli au adhabu”, ilisema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Katibu wa Kijichi Gharib S. Salim.
Aidha Kijichi ilidai kuwa, muamuzi huyo mwenye beji ya FIFA, alizikataa penelti mbili za dhahiri dhidi ya Mtende Rangers, ambapo katika kipindi cha kwanza, beki mmoja wa wapinzani wao aliukamata mpira kwa makusudi wakati ukielekea golini, na baadae mchezaji huyo huyo aliushika mpira katika eneo la hatari, bila muamuzi kumuadhibu.
Kijichi ilibainisha zaidi kuwa muamuzi huyo alishindwa kuwalinda wachezaji wake waliokuwa wakifanyiwa rafu mbaya na za makusudi, hali iliyoifanya kucheza mechi hiyo katika wakati mgumu na kukosa amani.
Uongozi huo ulieleza kuwa, unaamini kwamba muamuzi huyo alifanya hujuma kwa makusudi na sio kwa kutokujua, na kusema vitendo hivyo ni aibu kwa ZFA, Kamati ya Waamuzi Zanzibar na Shirikisho la Soka Duniani(FIFA).
Kutokana na sababu hizo, Kijichi Stars imeiomba ZFA na Kamati ya Waamuzi kulifanyia kazi tatizo hilo na kuchukua hatua kwa waamuzi wanaokiuka sheria na kanuni za kuchezesha mpira wa miguu
No comments:
Post a Comment