NAIBU waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, Charles Kitwanga amesema dira ya maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025 itafikiwa kwa haraka na kwa ufanisi endapo matumizi ya kisasa ya teknolojia ya habari na mawasiliano yatapewa kipaumbele.
Naibu huyo alieleza hao jana kwa niaba ya waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolijia Prof. Makame Mnyaa Mbarawa kwenye ufunguzi wa mkutano wa wa tatu wa uliozungumzia maendeleo ya Habari na mawasiliano ya Afrika (AFRICOMM) uliofanyika katika hoteli ya Zanzibar Ocean View iliyopo Kilimani mjini hapa.
Kitwanga alisema kasi ya maendeleo ya dunia kwa kiasi kikubwa imekuwa ikiendeshwa na kutegemea maendeleo ya sayansi na teknolojia, hivyo Tanzania nayo itaweza kuifikia dira yake ya maendeleo endapo itajikita kisawa sawa katika matumizi ya habari na Mawasiliano.
Alifahamisha kuwa katika kulifahamu hilo, serikali kwa upande wake imekuwa ikichukua jitihada mbali mbali za kurahisisha matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
“Serikali itaendelea kuwasaidia na kuwaunga mkono watafiti hasa katika eneo la teknolojia ya habari na mawasiliano”,alisema Kitwanga.
Alifahamisha kuwa tafiti zitakazofanywa juu ya kada ya teknolojia ya habari na mawasiliano zitasaidia kuondosha matatizo mbali mbali yanayoikabili jamii sambamba na kusukuma kazi ya maendeleo yao.
Kitwanga alivitaka Vyuo vikuu nchini kujiingiza kwenye tafiti hasa katika sekta hiyo kwani kwa kiasi kikubwa zitaiwezesha nchi kuwa na wataalamu wengi.
Alisema serikali imetenga fedha za kutosha asilimia moja ya fedha za pato la taifa ambazo zitatumika kwa ajili ya tafiti na kuvitaka vyuo vichangamkie fursa hiyo muhimu.
Aidha Naibu huyo, alisema kwa kiasi kikubwa Tanzania iko kwenye hatua nzuri katika matumizi ya teknolojia ya mawasiliano kwani hivi sasa kuna makampuni kadhaa ya simu huku kiasi cha wateja milioni 21 wa simu za mkononi wakiwa wameshasajiliwa.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar Prof. Idris Rai moja ya mipango iliyopo katika chuo hicho ni kuendeleza taaluma ya habari na mawasiliano.
Alisema ulimwengu kasi ya maendeleo ya ulimwengu na Zanzibar kama sehemu ya ulimwengu lazima iwe na wataalamu wengi habari na mawasiliano ambapo chuo hicho kitawapika wataalamu hao.
No comments:
Post a Comment