SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar na Ras Al Khaimah zimetiliana saini Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano katika uimarishaji wa sekta za maendeleo ambapo miongoni mwa makubaliano hayo ni pamoja na mashirikiano katika kuwawezesha wananchi wa Zanzibar kiuchumi na kuendeleza ajira.
Utiliaji saini huo ulishuhudiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na mwenyeji wake kiongozi wa Ras Al Khaimah Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi na viongozi wengine wa pande mbili hizo, huko katika ukumbi wa Kasri ya kiongozi huyo iliyopo mjini Ras Al Khaimah..
Kwa upande wa Zazibar Waziri wa Kazi, Uwezeshaji , Wananchi Kiuchumi na Ushirika Mhe. Haroun Ali Suleiman alisaini ambapo kwa upande wa Ras-Al-Khaimah aliyetia saini ni Sheikh Abdalla Bin Humaid Al Qasimi.
Miongoni mwa makubaliano hayo ni pamoja na kuendeleza Maeneo Huru ya Uchumi, Bandari Huru ambapo itaifanya Zanzibar kuwa Kituo Kikuu cha Biashara, ushirikiano wa kitaalamu, kuendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu katika nyanja za afya, nishati, huduma za afya, ufundi.
Aidha, utafiti juu ya vianzio vya maji, mashirikiano na serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuwawezesha wananchi Kiuchumi na kuendeleza ajira.
Mapema Dk. Shein alifanya mazungumzo na mwenyeji wake kiongozi wa Ras-Al-Khaimah Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi yaliolenga kukuza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo.
Mazungumzo hayo yaliofanyika katika Kasri ya Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi ililopo mjini Ras-Al-Khaimah, viongozi hao kwa pamoja walieleza haja ya kukuza uhusiano na kuimarisha mashirikiano katika kuinua seka za maendeleo ikiwemo uwekezaji, biashara, viwanda, elimu, Maeneo huru ya Uchumi, Afya na Uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Aidha, viongozi hao walizungumza juu ya sekta za maendeleona katika kuimarisha mashirikiano kwenye sekta nzima ya maeneo huru na uwekezaji sanjari na bandari huru.
Katika maelezo yake Dk. Shein alitoa shukrani kwa kiongozi huyo kutokana na mwaliko wake na kusisitiza kupongeza mafanikio yaliopatikana nchini humo kwa kipindi kifupi.
Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka kwa ndugu zao wa Ras-Al-Khaimah.
Nae Kiongozi huyo alieleza kuwa Ras-AlKhaimah itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar hasa katika sekta hizo za maendeleo.
Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar na Ras-el-Khaimah zina historia kubwa katika nyanja ya kibiashara hivyo hatua zaidi zitaimarishwa kwa pamoja katika kukuza sekta hiyo pamoja na sekta ya uwekezaji.
Pia, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Jumuiya ya Wafanyabishara wa Ras-Al-Khaimah na kueleza kuwa muendelezo wa biashara kati ya Zanzibar na Ras-Al-Khaimah ndio msingi kubwa ya uhusiano uliopo.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kupata maelezo kutoka kwa Jumuiya ya Wafanyabishara wa Ras-Al-Khaimah
Alieleza kuwa ziara hiyo imelenga katika kukuza uhusiano wa kibiashara, viwanda, uwekezaji kati ya Ras-Al-Khaiman na Zanzibar. Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina vivutio vingi vya Utalii ambapo juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na serikali katika kuiimarisha sekta hiyo.
Wakitoa maelezo yao wafanyabishara hao walieleza kuwa Ras-Al-Khaimah ina mambo mengi ya kushirikiana na Zanzibar na kusisitiza kuwa iko tayari kuendeleza uhusiano na udugu wao kwa kuimarisha sekta za maendeleo.
Walieleza kuwa miongoni mwa sekta ambazo wako tayari kushirikiana ni pamoja na sekta za uwekezaji, viwanda, biashara na nyenginezo na kusisitiza kuwa Zanzibar imeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika sekta ya Utalii, hivyo nao wana mengi ya kujifunza kutoka Zanzibar.
Nayo Hospitali Kuu ya Rufaa ya Ras Al Khaimah imeahidi ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katka kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na azma ya kusaini makubaliano ya kushirikiana katika kutoa huduma za upasuaji kwa maradhi ya figo, moyo, saratani na mengineyo.
Dk. Shein akiwa na ujumbe wake pia, alitembelea Chuo Kikuu cha Sayansi cha Ras-Al-Khaimah, Hospitali ya rufaa ya Ras-Al-Khaimah pamoja na kutembelea kiwanda cha dawa cha JULPHAR, alitembelea Maeneo Huru ya uwekezaji RAKIA ambako hutengeneza bidhaa mbali mbali zikiwemo tiles, vyombo vya nyumbani na vyenginevyo.
No comments:
Post a Comment