HATIMAYE Stewart John Hall, ameamua kukitema kibarua chake cha kuinoa timu ya soka ya taifa 'The Zanzibar Heroes'.
Hatua hiyo inafuatia wiki mbili za utata kuhusu kocha huyo kushindwa kuifuata timu hiyo jijini Cairo Misri, ilikokuwa imepiga kambi kujiandaa kwa ajili ya michuano ya Chalenji inayotarajiwa kuanza kesho jijini Dar es Salaam.
Muingereza huyo alikwama kwenda Misri kwa kile kilichoelezwa kuwa paspoti yake ilikuwa imejaa na kukosa ukurasa wa kugonga viza ya nchi hiyo.
Kocha huyo alilipigia simu gazeti hili mapema jana, na kuliambia kuwa ameamua kuipa kisogo timu hiyo, akikataa masharti aliyopewa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), ili abakie kuwemo katika benchi la ufundi la timu hiyo.
Akiyataja masharti hayo, Stewart ambaye pia ni kocha wa klabu ya ligi kuu Tanzania Bara Azam FC, alidai ametakiwa kuwaachia makocha Hemed Suleiman 'Moroko' pamoja na Abdelfatah Abbas kuiongoza timu hiyio katika Chalenji, naye akiagizwa kuwa mshauri wa ufundi hadi katika
mashindano mengine yatakayofuata.
"Nilipoelezwa hivyo, baada ya ZFA kuamua, niliomba muda wa saa moja ili nifikiri, lakini nimekata shauri kuachana na timu hiyo", alifafanua.
Hata hivyo, alisema licha ya kuitema Zanzibar Heroes, moyo wake wote uko pamoja nayo katika michuano hiyo, na kwamba anaiombea kila la kheri ili iweze kutwaa ubingwa.
Zanzibar Leo iliwasiliana na Katibu Mkuu wa ZFA Mzee Zam Ali kutaka ithibati iwapo kocha huyo amekiarifu azma ya kujiuzulu, lakini akaagiza atafutwe mwajiri wake kampuni ya Future Century, ambayo ilikiri kutumiwa ujumbe kwa njia ya mtandao kutoka kwa Stewart, akisema ameona ni vyema akae kando baada ya ZFA kudai haiwezi kumtumia kwa vile anaweza kuwachanganya wachezaji ambao hayuko nao tangu awali.
No comments:
Post a Comment