Habari za Punde

Maalim Seif Akutana na Jumuiya ya Wafanyabiashara na Kupambana na Ukimwi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Fatma Abdulhabib Fereji akibadilishana mawazo na wataalamu wa masuala ya UKIMWI na afya ya jamii kutoka Marekani waliofika ofisini kwake Migombani kwa ajili ya kuzungumza nae. Wataalamu hao ni Bibi Irene Benech na Richied Needh (Picha, Salmin Said, OMKR).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na wajumbe wa kamati tendaji wa jumuiya ya ABCZ walipofika ofisni kwake Migombani mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na kupambana na UKIMWI Zanzibar ABCZ Bwana Ali Aboud Mzee, wakati wajumbe wa kamati tendaji wa jumuiya hiyo walipofika OMKR migombani kwa ajili ya kujitambulisha.


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema serikali inafarajika kuona taasisi binafsi zinapata mwamko wa kushikiana nayo katika kutekeleza majukumu yake.

Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kusogeza mbele harakati za maendeleo na kutatua kero zinazowakabili wananchi na taifa kwa jumla.

Maalim Seif ameeleza hayo leo huko ofisini kwake migombani alipokuwa na mazungumzo na wajumbe wa kamati tendaji kutoka Jumuiya ya wafanyabiashara na kupambana na UKIMWI Zanzibar (ABCZ) waliofika kwa ajili ya kutambulisha.


Amesema mapambano dhidi ya UKIMWI sio jukumu la serikali pekee, hivyo taasisi binafsi na wananchi hawana budi kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya janga hilo.

“Ikiwa hatutokuwa makini janga hili la UKIMWI linaweza kuliangamiza taifa letu, na sisi hatuko tayari kwa hilo, hivyo hatuna budi wadau wote tushirikiane juu ya jambo hili.” Alisema Maalim Seif.

Amesema serikali kwa sasa imo katika mkakati wa kuzuia maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI ili kulilinda taifa kupoteza nguvu kazi ya vijana ambao ndio waathirika wakubwa wa janga hilo.

Katika hatua nyengine Makamu wa Kwanza wa Rais ameitaka jamii kushirikiana juu ya suala la malezi ili kuwajenga watoto katika maadili mema, na kwamba hatua hiyo pia itasaidia kujikinga na maambukizi mapya.

“Maadili yameporomoka sana katika jamii yetu, hivyo jamii nayo ishirikiane katika malezi ili kurejesha maadili yetu. Wazazi na walezi nao wachukue jukumu lao katika kuwaandaa watoto kenye malezi mema na sio kuitupia lawama serikali” alitanabahisha.

Kwa upande wake mwenyekiti wa jumuiya hiyo ya ABCZ bwana Ali Aboud Mzee amesema mbali ya mapambano dhidi ya UKIMWI, jumuiya hiyo pia inakusudia kufanya kazi za ziada za kijamii zikiwemo mazingira na kupambana na umaskini.

Amepongeza mashirikiano wanayoyapata kutoka serikalini juu ya utekelezaji wa malengo yao na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo kwa lengo la kufikia malengo yao ambayo ni pamoja na kuifikia jamii kubwa zaidi hadi ngazi za familia.

Wakati huo huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Fatma Abdulhabib Fereji amekutana na wataalamu wa masuala ya UKIMWI na afya ya jamii kutoka Marekani na kuahidi kushirikiana nao katika masuala mbali mbali yakiwemo UMIMWI na dawa za kulevya.

Mhe. Fereji amesema wakati serikali inajidhatiti kuwakusanya vijana walioamua kuachana na matumizi ya dawa za kulevya, bado wanakabiliwa na changamoto nyingi katika kuziendesha Sober Houses zipatazo kumi Unguja na Pemba.

Hassan Hamad (OMKR).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.