Habari za Punde

'Mapinduzi Cup' Imetuchonga Ukali-Shija

Na Masanja Mabula

KUSHIRIKI katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi, kumechukuliwa na klabu ya Jamhuri kuwa ni kigezo cha kutambua mapungufu na kupata makali ya kuwashinda wapinzani wao kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Jamhuri ambao ni wawakilishi wa Zanzibar kwenye michunao hiyo ya Afrika, inatarajiwa kushika dimbani Gombani kwa mcezo wa kwanza Februari 18, mwaka huu kuikabili timu ya Hwange kutoka Zimbabwe.


Mara baada ya kuwasili kisiwani Pemba na kupokelewa na mamia ya mashabiki wao, Kocha Mkuu wa timu hiyo Renatus Shija, alisema michuano hiyo imewasaidia kuona ni wapi kwenye kasoro, na kuongeza kuwa baada ya kufahamu, anajipanga kuyafanyia kazi mapungufu yote yaliyojitokeza wakati wa ngarambe hizo za siku tisa.

"Kwa kweli mashindano yale yalikuwa sawa na darsa kwetu, tumejifunza na kufahamu kasoro kadhaa, ambazo sasa tunataka kuzirekebisha kabla kutia mguu kwenye kinyang'anyiro cha CAF", alieleza Shija.

Aidha aliwasifia wanandinga wake kwa uwezo mkubwa walioonesha kwenye patashika hiyo, ampapo haikupoteza mchezo katika hatua ya makundi na kuweza kufika fainali ambapo ilichapwa na Azam FC mabao 3-1.

"Pamoja na hamu yetu kutwaa ubingwa, tuliyatumia mashindano ya Mapinduzi kama sehemu ya maandalizi kabla michuano ya CAF, na kwa kweli vijana wamekomaa na kunipa matumaini ya kupambana vyema huko twendako", alijigamba kocha huyo.

Nao mashabiki waliofika kukipokea kikosi hicho, waliipongeza timu hiyo kwa hatua iliyofikia, na kusema kiwango kilichooneshwa na wachezaji hao, kimewapa matumaini makubwa ya kufanya vyema katika michuano ya Kombe la Shirikisho pamoja na ligi kuu ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.