Habari za Punde

Mkaazi wa Konde Adakwa na Polo la Bangi

Na Masanja Mabula, Pemba

JESHI la Polisi mkoa wa Kaskazini Pemba, linamshikilia mkaazi wa Konde, Seif Juma Seif (52) baada ya kukutwa na polo lenye mafurushi 62 ya majani makavu yanayosadikiwa kuwa ni bangi.

Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Polisi mkoa huo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Yahya Rashid Bugi alisema polisi imefanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa huyo kutokana na msaada mkubwa wa
polisi jamii.


Alisema ilikuwa kazi rahisi kwa askari wa jeshi lake kumtia mikononi baada ya taarifa kutoka kwa raia wema waliopenyeza habari za bangi hiyo.

Alifahamisha kuwa baada ya kupokea taarifa kutoka kwa raia wema, kikosi cha polisi kutoka Makao Makuu ya Mkoa walipiga kambi kwa siku tatu na kuweka mtego uliohakikisha unamtia mikononi mtuhumiwa huyo.

Kamanda Bugi alisema mtuhumiwa alikamatwa juzi majira ya saa 4 usiku ambapo mara baada ya kukamatwa aliwashawishi askari kwa kuwapa rushwa ya shilingi 900,000 ili wamuachilie.

“Mtuhumiwa alipokamatwa na Polisi aliwashawishi kwa kutaka kuwapa rushwa ya shilingi 900,000 ili wamuachie, ambapo walimtaka asubiri hadi kupambazuke na ilipofika asubuhi walimtia pingu na kumfikisha
kituo cha Polisi Konde”, alisema Kamanda huyo.

Alisema jeshi hilo mbali ya kumshitaki kwa tuhuma za kukamatwa na polo lenye mafurushi hayo ya bangi, pia litamfungulia mashitaka ya kushawishi kutoa rushwa.

Bugi amewaomba wananchi kushirikiana na jeshi lake kwa kulipatia habari mbali mbali za uhalifu ili waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyomvo vya sheria.

Alisema jeshi lake liko kwa ajili ya kulinda raia na mali zao na wale watakaopenyeza siri za uhalifu watalindwa na kuhakikisha kuwa taarifa zao hazivuji.

Katika tukio jengine mkaazi wa Kiuyu Koongo, Asha Shehe Shamata (45), amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia shuka la kitandani.

Kwa mujibu wa Kamanda Bugi alisema tukio hilo lilitokea juzi ambapo mume wa marehemu huyo alisikia mshindo wa kuanguka kiti na alipofika alimkuta mkewe akiwa ameshakufa.

Alisema hakuna taarifa kuwa marehemu alikuwa na matatizo ya kiafya na kwamba hakuacha ujumbe wowote ambapo baada ya uchunguzi mwili huo ulizikwa jana huko Kitambuu, Mchangamdogo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.