MKE wa Makamu wa Pili wa Rais, Mama Asha Seif Iddi, ameitaka jamii kujitolea kuwawezesha walimu wa vyuo vya madrasa ili wawe na majengo ya kisasa ya kufundishia elimu ya Qur-aani, badala ya kuwaacha kutumia kumbi za nyumba zao ama mabanda yasio
Mama Asha aliyasema hayo jana wakati akitoa nasaha zake katika maulidi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W), yaliotayarishwa na Madrasa Al Imaniya ya Makadara Mjini Zanzibar.
Mama Asha, alisema jamii inapaswa kuanza kuliona hilo kutokana na hivi sasa kuonekana majengo mengi yanayotumika kwa ajili ya kutoa elimu ya Qur-ani, ni yenye kuchakaa huku yakiwa yanakosa huduma bora za kulinda afya za wanafunzi.
Kutokana na hali hiyo Mama Asha alisema, mfumo uliozeleka wa kutumia kumbi za nyumba za walimu ama vipenu unahitaji jamii ya kiislamu kushiriki kuubadili ili uweze kuwapa faraja wanafunzi wanaotumia madrasa hizo.
Alisema hivi sasa wengi wa waislamu wamekuwa wakijitolea kujenga misikiti ikiwemo ya ghorofa, lakini upande mwengine wamekuwa wagumu kujitolea kujenga madrasa za kisasa.
Alisema huo sio mwenendo bora kwani ili muumini aweze kuufikia msikiti huo anahitaji kupata elimu ya dini ya kiislamu ambayo msingi wake hutolewa katika madrasa.
Kutokana na hali hiyo Mama Asha, aliiomba jamii ya kiislamu kulifikiria suala la kuzipa hadhi madrasa kwa kujitolea kuzijenga na kuzipatia vifaa vya kisasa.
Mama Asha, akiendelea pia aliitaka jamii ya kiislamu kuwa na tabia ya kupendana ikiwa ni kuendeleza mwenendo bora wa Mtume Muhammad (S.A.W) na sio kutendeana ubaya kama inavyojitokeza katika jamii hivi sasa.
Alisema inasikitisha hivi sasa kuna baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu wamekuwa wakigombana wenyewe kwa wenyewe huku baadhi ya familia kufikia kutendeana vitendo vibaya.
Hali hizo Mama Asha, alisema zinaenda kinyume na mwenendo wa Mtume Muhammad, na ni vyema jamii ya kiislamu kuanza kuiona hatari hiyo na kuiepuka ili waweze kuendeleza mbele mema ya Mtume Muhammad (S.A.W)
Hata hivyo, aliwaasa wazazi kuwapa ushirikiano walimu wa madrasa kwa kuona wanawapatia michango ya ada ili kuwawezesha walimu hao kumudu sehemu ya maisha yao kwa vile muda mwingi hulazimika kuutumia kuwapa elimu ya akhera watoto wao.
No comments:
Post a Comment