Habari za Punde

Tafuteni Ufumbuzi Tatizo la Ujenzi wa Kituo cha Polisi Sebleni - Balozi Seif


Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Maendeleo ya Makaazi, Maji na Nishati Nd. Mwalimu Ali Mwalimu akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kuhusu waya Mkubwa wa Umeme ulioko chini ya Ardhi ambao uko sambamba na msingi wa ujenzi wa Kituo cha Polisi kiliopo Sebleni Muungano.
Kulia yao ni Meneja wa Shirika la Umeme Zanzibar { Zeco } Nd. Hassan Ali Hassan, Mbunge wa Jimbo la Amani Mh. Mussa Hassan Mussa. Kushoto yao ni Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moh’d Aboud Moh’d na Mkurugenzi Ardhi Nd. January Fusi.


Mawaziri wa Wizara za Miundo Mbinu, Ardhi, Maendeleo ya Makaazi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi pamoja na Uongozi wa Jimbo la Amani wameagizwa kukaa pamoja kulitafutia ufumbuzi tatizo la ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Sebleni Muungano ambao Umejitokea kuwa na utata katika Ujenzi wake.

Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati alipofanya ziara ya ghafla kukagua eneo la ujenzi wa Jengo la kituo hicho ambao uko katika ngazi ya Msingi.


Balozi Seif alishuhudia hitilafu za ujenzi huo ambao umeikumba pia Bomba ya Waya za Umeme wa Chini kwa Chini unaosambaza huduma hiyo ukanda wa Magharibi pamoja na Mpango wa Ujenzi wa Bara Bara Kuu itokayo Mtaa wa Kwa Boko kuelekea Muungano.

Alisema ni vyema yakazingatiwa matakwa ya Wananchi katika masuala ya Jamii bila ya kuharibu taratibu zilizopo za Mipango Miji ambazo huonekana kuvurugwa na baadhi ya Watu.

Aliziagiza pande hizo mbili kuhakikisha kwamba ufumbuzi wa suala hilo unapatikana ndani ya pindi cha wiki moja.

Balozi Seif aliendelea kuwaasa watu wenye tabia ya kuvamia maeneo ya wazi kwa ajili ya ujenzi kuacha kuendeleza tabia hiyo ambayo huiletea hasara kubwa Serikali Kuu wakati inapofikia maamuzi ya kutandika Miundo mbinu.

“ Tabia ya baadhi ya watu kusubiri kujengwa kwa Majengo ya shughuli za Kijamii na wao kuanzisha kajengo yao bila ya kuzingatia taratibu za Ujenzi hivi sasa umekuwa sugu katika maeneo mengi hasa yale ya wazi”. Alifafanua Balozi Seif.

Mapema Mwakilishi wa Jimbo la Amani Mh. Fatma Mbarouk Said alisema Uongozi wa Jimbo hilo kwa Kushirikiana na Wananchi umefikia hatua ya kujenga Kituo cha Polisi kutokana na madhila wanayoyapata Wananchi hasa nyakati za usiku.Mh. Fatma alisema kumekuwa na vitendo viovu wanavyofanyiwa Wananchi wakati wakipita maeneo hayo likiwemo suala la ubakaji na hata unyang’anywi wa vitu na mali zao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Maendeleo ya Makaazi, Maji na Nishati Nd. Mwalimu Ali Mwalim alisema Ujenzi wa msingi wa kituo hicho uko sambamba na waya mkubwa wa umeme ulioko chini ya ardhi.

Ndugu Mwalimu alimueleza Balozi Seif kwamba ujenzi huo unaweza kuleta athari endapo taratibu sahihi za matumizi ya eneo hilo hazitazingatiwa vyema.

Eneo la Ujenzi wa Kituo cha Polisi Sebleni Muungano licha ya kuwa na umeme mkubwa wa chini ya ardhi unaosambaza huduma hiyo katika kanda ya magharibi ya Kisiwa cha Unguja lakini pia limo katika mipango Miji ya Kupitishwa ujenzi wa Bara Bara Kuu itokayo Muungano hadi Kwa Boko.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar
27/3/2012.

1 comment:

  1. This comment has been removed by a blog administrator.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.