WAKAAZI wa Shehia ya Ndijani Mseweni, wanakabiliwa na tatizo la muda mrefu la upatikanaji wa maji safi na salama ndani ya shehiya yao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mkaazi wa Mseweni Abdalla Rashid Gungwa, alisema kuwa tatizo hilo limedumu kwa takiban miaka mitatu sasa.
Alisema wananchi Mseweni hasa akina mama wamekuwa wakisumbuka kuisaka huduma hiyo muhimu ambayo imekuwa ikipatikana kwenye baadhi ya visima vya asili.
“Tatizo hili la maji safi na salama limekuwa ni la muda mrefu kwani linatupa usumbufu na kuzorotesha shughuli za maendeleo kwa kutumia muda mwingi kutafuta maji kwa ajili ya matumizi muhimu”, alisema Gungwa.
Hata hivyo aliiomba Mamlaka ya maji ZAWA kuwatatulia tatizo hilo kwa haraka ili waweze kuondokana na usumbufu.
Kwa upande wake ofisa uhusiano Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Zahor Suleiman Khatib alisema Mamlaka yake iko mbioni kulishughulukia suala hilo kwa kutafuta eneo muafaka litakalo tumika kuchimba kisima.
Ofisa huyo aliwaomba wafadhili mbali mbali kuwasaidia katika suala hilo la kuleta maji safi na salama ndani ya shehiya ya Ndijani Mseweni.
Zahor alitoa wito kwa wananchi wanaopata huduma hiyo kuchangia kwa lengo la kuimarisha huduma hiyo kwani kufanya hivyo watakuwa wamesaidia serikali katika upatikanaji wa huduma mbali mbali hapa nchini.
0 Comments