Habari za Punde

Vikosi SMZ vyatakiwa kuunga mkono “Polisi Jamii”

Na Ramadhan Himid, POLISI

KAMISHNA wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa amewataka Maofisa na Askari wa Kikosi cha Magereza na Zimamoto kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa dhana ya Polisi Jamii ili kupunguza kero mbali mbali za Uhalifu katika maeneo wanayoishi.

Kamishna Mussa alitoa wito huo kwa Maafisa na Askari walioko kwenye mafunzo katika Chuo cha Magereza Hanyegwamchana Wilaya ya Kati Unguja ikiwa ni moja katika mkakati wa Jeshi hilo kuieneza dhana ya Polisi Jamii katika taasisi zote za Serikali.


Alisema dhana ya Polisi Jamii haikuja kwa bahati mbaya bali inatokana na maboresho yanayoendelea kufanywa ndani ya Jeshi hilo katika kutekeleza majukumu yake kikamilifu, ambapo maboresho hayo yanalenga katika mihimili mikuu mitatu, yaani Ueledi, Usasa na Polisi Jamii.

Aidha alisema dhana ya Polisi Jamii ni kongwe duniani kote ambapo ilianzishwa na Mtaalamu Robert Peel miaka ya 1800 nchini Uiengereza na ilileta tija kubwa katika kupunguza uhalifu na hivyo basi kila mtu anawajibika kuikubali na kuifuata bila kujali rangi, chama, kabila ,au dini.

Alisema taifa lolote lenye uhalifu watu wake hawawezi kuwa na fikra za kimaendeleo na badala yake watatumia muda mwingi katika kuutatua uhalifu huo, hivyo ni vyema kila mmoja ndani ya jamii kuhakikisha anachukizwa na uhalifu ili kujiletea maendeleo endelevu.

Aliwaambia wapiganaji hao kuwa maana ya Polisi Jamii ni ushirikishwaji wa kila mtu aliyekuwemo ndani ya jamii zetu itategemea na nafasi aliyonayo mtu huyo kwa lengo zima la kupunguza kero mbali mbali za uhalifu na kuleta ustawi wa jamii.

Alisema dhana ya Polisi Jamii ina miradi mingi ikiwemo mradi wa utii bila shuruti kwa kuwataka wananchi kutii sheria za nchi bila kusubiri kushurutishwa, kwani kushurutishwa kufanya jambo kuna gharama kubwa mno.

Mradi mwengine ni Ulinzi Shirikishi kwa kuwashajihisha wananchi kuunda Vikundi vya Sungusungu katika maeneo yao wanayoishi ili kupunguza kero za uhalifu.Katika mradi huu amewaomba Askari hao kujiunga katika vikundi hivyo katika maeneo yao kwani wao wana msaada mkubwa kwa kuwa wana taaluma ya uaskari, hivyo wanaweza kusaidia kutatua kero hizo ndani ya Shehia zao.

Aliutaja mradi mwengine kuwa ni Ulinzi Jirani ambao unawataka wananchi waishi katika ujirani mwema kwa kupeana mikakati imara ya kupunguza uhalifu katika maeneo yao wanayoishi ikiwemo kupeana taarifa pale mmoja anapoondoka ili kumsaidia jirani yake kumlindia mali yake pale anapoondoka

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.