Habari za Punde

Makamanda Wapigwa ‘stop’ Kudokoa Mishahara ya Askari

Na Mwantanga AmePublish Post

SERIKALI ya Zanzibar imewataka Makamanda wa Idara Maalum, kuacha mara moja kuwakata askari wao mishahara yao kwa ajili ya kuchangia mambo mbali mbali ya taasisi hizo.

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame, aliyasema hayo mbele ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kikao ambacho kinaendelea mjini hapa.

Kauli ya Waziri huyo imekuja baada ya baadhi ya Wajumbe wa Baraza hilo kuhoji ni kwanini wizara hiyo imekuwa ikiwakata askari fedha zao za mshahara wakati wakijua mshahara ni mali ya muajiriwa na haupaswi kukatwa bila ya idhini yake.

Wajumbe waliohoji wizara hiyo ni pamoja na Hijja Hassan Hija Mwakilishi wa Kiwani, Mwakilishi wa Jimbo la Kitope, Makame Mshimba Mbarouk na Ismail Jussa Ladhu ambapo walitaka kujua kwa nini serikali imekuwa ikiendeleza mpango huo bila ya ridhaa ya wafanyakazi hao.

Walisema wafanyakazi hao wamekuwa wakikatwa fedha katika mishahara yao ambazo hutumika kuchangia michezo jambo ambalo halijulikani kama ni lazima ama ni la hiari huku kukiwa hakuna hatua zinazoleweka katika upandishaji wa vyeo kwa askari hao.

Dk. Mwinyihaji alisema ni kweli hapo awali kulikuwa na tatizo hilo lakini hivi sasa tayari wamefanya mazungumzo na Makamanda wa vikosi hivyo kuacha utaratibu huo.

Alisema waliamua kuchukua hatua hiyo kwa kutambua mshahara wa mfanyakazi ni mali yake na haiwezekani kulazimishwa kuchangia kitu bila ya ridhaa yake kwani kufanya hivyo ni kinyume na kanuni za utumishi.

Alisema kisheria hakuna mtu yoyote wa serikali anaetakiwa kukatwa mshahara wake bila ya idhini yake isipokuwa kama kumewekwa utaratibu wa kufanya hivyo baada ya muhusika kujulishwa.

Alisema wanachokusudia kukifanya ni kuona makamanda hao wanatii amri hiyo ya serikali kwani bado hawatakiwi kuendesha utaratibu huo kutoka katika mshaahara wa mfanyakazi.

Alisema katika miaka ya nyuma Idara Maalum za SMZ waliweka utaratibu wa kuwakata posho ya chakula askari wa taasisi hizo kwa wanaolala kambini na wanaoenda mafunzoni ambao ni utaratibu wa kawaida.

Hata hivyo alisema serikali baadae iliamua kuusitisha baada ya kuona unazidisha mzigo kwa watumishi wa Idara maalum na kuamua kuziingiza fedha hizo katika bajeti zao ambazo mfanyakazi huzipata katika mshahara wake.

Akizungumzia kwa upande wa michango ya sekta ya Michezo Waziri huyo alisema michango yake hupatikana kutoka kwa watumishi wa Idara hizo kujitolea kwa hiari yao wao wenyewe kwa lengo la kuziendeleza klabu zao.

Kuhusu utaratibu wa kupandisha vyeo, waziri huyo alisema hufanywa na Tume ya Utumishi ya Idara Maalum za SMZ, baada ya kuangalia sifa na vigezo vya upandishaji wa vyeo hivyo.

Hata hivyo akizungumzia juu ya suala la fedha za uhamisho alisema tayari alishatoa maelekezo kwa Makamanda wa vikosi kuhakikisha wanaomadai hayo yanashughulikiwa kwa haraka.

Aidha, Waziri huyo alikiri kuwapo kwa makaazi duni ya askari hasa kisiwani Pemba katika kambi ya Kangagani ambapo alisema itawashughulikia tatizo hilo.

Idara maalum zilizokuwemo chini ya Wizara hiyo ni pamoja na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Kikosi cha Kuzuiya Magendo (KMKM), Askari wa VALANTIA (KVZ)na Kikosi cha Uokozi.

Nae Mwanasheria Mkuu wa serikali Othman Masoud, alilomba baraza hilo kuurejesha Mswada uliokuwa ukitarajiwa kuwasilishwa juzi washeria na Marekebisho ya sheria mbali mbali na kuweka masharti yaliomo ndani yake.

Mwanasheria huyo alisema ameamua kuurejesha mswada huo katika Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala kwa lengo la kuingiza baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na wadau ambayo hayakuwemo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.