Habari za Punde

Sayansi Hurahisisha Usalama, Afya Kazini – Waziri Haroun

Na Kauthar Abdalla

WAZIRI wa Kazi, Uwezeshaji, Wananchi, Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman amesema kukua kwa sayansi na teknolojia kunarahisisha utoaji wa huduma za usalama na afya kwa wafanyakazi wawapo kazini licha ya changamoto mbali mbali zinazowakabili.

Akitoa taarifa maalum kuhusiana na maadhimisho ya siku ya usalama na afya kazini duniani, alisema kwa upande mmoja au mwengine sehemu za kazi kunakuwepo changamoto nyingi zinazohatarisha usalama na afya za wafanyakazi, jamii na mazingira kwa ujumla.

Waziri alisema changamoto kubwa zaidi ni madhara ya kiafya yanayoweza kuonekana mara moja na yale yanayochukua miaka kujulikana jambo ambalo huhatarisha maisha ya watu wengi kwa kile kipindi ambacho wanakuwa katika maeneo ya kazi.

Aidha alifahamisha kuwa mazingira bora ya kazi hurahisisha uzalishaji na hivyo pato la muajiri, muajiriwa na mataifa mbali mbali kwa jumla ambapo kwa maana halisi ni kuwa mazingira bora ya Kazi hukuza pato la uchumi wa nchi.

Alisema kuwa mambo ya usalama na afya kazini yanaposimamiwa ipasavyo ni vyema kwa wafanyakazi kwani watafanyakazi kwa usalama wakiwa na afya njema pia mashine, mitambo na vifaa vitatumika kwa ufanisi na kutoa tija zaidi.

Haroun alisema kuwa vifaa vibovu visivyofanyiwa matengenezo kwa wakati unaotakiwa ni hatari kwa wafanyakazi,waajiri na jamii kwa jumla ambapo hupelekea uzalishaji mdogo unaosimama mara kwa mara na bidhaa au huduma zilizo chini ya kiwango.

Alifafanua kuwa ili kuweka uwiano wa mambo hayo shirika la Kazi Duniani (ILO) limetunga mikataba na mapendekezo mengi,tokea kuanzishwa kwake mwaka 1919 juu ya usalama na Afya Kazini ambapo pia kwa upande wa Zanzibar inayo sheria namba 8,ya mwaka 2005.

Pia watendaji na wawajibikaji wakubwa katika sheria hiyo wataonekana zaidi katika hali bora za wafanyakazi wenye Afya nnjema na hamasa ya kufanya kazi nakupunguza ajali, maumivu, madhara, maradhi na vifo vitokanavyo na kazi.

Pamoja na kuweka usalama wa jamii na mazingira yanayozunguka sehemu za kazi na kuongeza pato la Taifa kutokana na sehemu za kazi kuwa na ufanisi na kutoa tija kubwa zaidi.

Hata hivyo alisema jamii inahitajika kufahamu umuhimu wa usalama na Afya kazini, uhusinao wake na maisha yao ya kila siku ambapo pia taaluma hiyo itasaidia kila kuhusika kujua haki na wajibu wake hasa pale taratibu za usalama na afya kazini zinapokiukwa na athari zinazoweza kupatikana.

Vile vile alisema kutokana na hali mbaya ya mazingira ya kazi yanasababisha wafanyakazi kuathirika na kupelekea kuwa na afya duni za Wafanyakzi wasioweza kuzalisha kiwango kile kinachotakiwa.

Pamoja na hayo alisema kuwa Usalama na Afya Kazini ni hifadhi ya wafanyakazi,waajiri,wamiliki wa sehemu za kazi na jamii kutokana na ajali na maradhi yanayotokea kwenye mazingira ya kazi.

Kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho hayo ni Uhamasishaji wa usalama na Afya kwenye kaiz zitakazokuwa salama kwa mazingira.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.