6/recent/ticker-posts

Simba Yatua Misri Salama Usalimini

CAIRO, Misri

KIKOSI cha timu ya Simba ambayo ni pekee kwa Tanzania inayoendelea na michuano ya Afrika, tayari kimewasili mjini Cairo, Misri kikiwa njiani kwenda Algeria.

Simba iliondoka alfajiri ya jana katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Dar es Salaam kuelekea Algeria kwa ajili ya mechi ya marudiano, raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Afrika dhidi ya ES Setif, wakipitia Cairo.

Wekundu hao, ambao kabla ya kuondoka nchini, waliifunga African Lyon mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom, waliondoka wakiwa na matumaini makubwa ya kuitoa ES Setif katika mchezo huo unaotarajiwa kufanyika Ijumaa ijayo.

Timu hiyo ina mpango wa kukaa kwa siku mbili katika mji mkuu wa Misri, Cairo kabla ya kupanda ndege itakayoichukua hadi Algeria.

Wachezaji waliomo kwenye msafara huo ni Juma Kaseja, Ally Mustafa, Nassor Masoud, Shomari Kapombe, Amir Maftaha, Juma Nyoso, Kelvin Yondani, Victor Costa, Obadia Mungusa, Jonas Mkude, Patrick Mafisango, Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi, Salum Machaku, Uhuru Suleiman, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Edward Christopher, Derick Walulya na Gervais Kago.

Msafara wa timu hiyo unajumuisha viongozi tisa, ambao ni Mwenyekiti Ismail Aden Rage, Mjumbe wa Kamati Tendaji Damian Manembe na Ofisa Habari, Ezekiel Kamwaga.

Wengine ni Kocha Mkuu, Milovan Cirkovic, Kocha Msaidizi Amatre Richard, kocha wa makipa James Kisaka, daktari wa timu Cosmas Kapinga, Meneja Nico Nyagawa na mtunza vifaa Kessy Rajab.

Simba ilishinda mchezo wa kwanza wiki moja iliyopita mabao 2-0, hivyo sare ya aina yoyote inatosha kuiopeleika hatua ijayo, au isifungwe zaidi ya bao 1-0 ikiwa ugenini.

Post a Comment

0 Comments