Habari za Punde

Tausi Taarab kwenda Misri, Lebanon


Itashiriki matamasha ya kimataifa

Na Aboud Mahmoud

KIKUNDI cha taarab kinachoundwa na wasanii wanawake, Tausi Women Taarab, kinatarajiwa kuondoka Zanzibar Aprili 24, kwenda katika nchi za Misri na Lebanon kwa ajili ya kushiriki matamasha mbali mbali ya muziki.

Mkurugenzi wa kikundi hicho Maryam Hamdan, amesema msafara wa wasanii hao utasafiri kwa ndege ya Shirika la Ethiopian Airline, ukijumuisha wanamuziki 11.

Maryam amefahamisha kuwa, tamasha la kwanza watakaloshiriki linaitwa ‘Spring Festival’ ambalo litafanyika katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut, Aprili 26.

Baadae, alifahamisha kuwa watasafiri hadi Misri ambako watafanya maonesho mawili katika miji tafauti, la kwanza likiwa Aprili 28 mjini Cairo, na jengine litafanyika Aprili 29 katika mji wa bandari Alexandria zaidi ya kilomita 400 kutoka Cairo.

Aliwataja wasanii watakaosafiri na kikundi hicho kuwa ni, pamoja naye akiwa kiongozi wa msafara, Fatma bint Baraka ‘Bi Kidude’, Sheria Issa, Topsy Surrie, Wahida Mohammed na Tabu Makame.

Wengine ni Tatu Khamis, Asha Khatib, Fatma Bakari, Mwaka Mshindo na Mohammed Ilyas ambae anakwenda akiwa mwalimu wa kikundi hicho.

Alieleza kuwa mialiko hiyo imekuja kutoka Kituo cha Utamaduni cha ‘Egypt Cultural Centre’ nchini Misri pamoja na ‘Shams Cultural Association’ ya Lebanon.

Mbali na Tausi, Maryam alisema matamasha hayo pia yatajumuisha wasanii na vikundi vya nchi nyengine ikiwemo Uingereza, Ujerumani, Iran, Syria, Tajikistan, Uholanzi na nyengine kadhaa.

“Tunaondoka tukitaraji kuipeperusha vyema bendera ya Zanzibar katika medani ya sanaa na utamaduni, kwani tumefanya mazoezi ya kutosha na tuko vizuri”, alisema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.