Habari za Punde

Viongozi Vinara wa Migogoro ya Ardhi

Kunze Mswanyama na Kawthar Iss-hack, DAR ES SAALAM

MIGOGORO mingi ya ardhi inatokana na baadhi ya viongozi waliopewa mamlaka ya kusimamia sekta hiyo kutowajibika ipasavyo katika nyadhifa zao jambo linalowasabibishia wananchi migongano.

Wakizungumza kwenye semina iliyoandaliwa na taasisi ya Haki Ardhi ya jijini Dar es salaam iliyozungumzia umiliki, matumizi, uwekezaji na migogoro ya ardhi nchini Tanzania, baadhi ya washiriki walisema migogoro hiyo ni ya kujitakia na ambayo imesababishwa na viongozi wasiowajibika ipasavyo.

Thomas John Laiser ambaye ni mwakilishi wa mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) alikitaka Kituo cha Uwekezaji cha Taifa (TIC), kutoa elimu zaidi juu ya umiliki wa ardhi kwa wenyeviti wa serikali za vijiji kwani wengi wao humiliki ardhi kinyume cha sheria pasipokuulizwa na yeyote.

Laiser aliongeza kuwa, sheria ya sasa ya ardhi inayombagua mwanamke kwenye umiliki wa ardhi ifanyiwe marekebisho ili kuondoa unyanyasaji huo dhidi ya kundi hilo nyonge.

Francis Uhadi ambaye ni Afisa Programu wa Haki ardhi alibainisha kuwa migogoro hiyo ambayo husababisha baadhi ya wananchi kuondolewa katika ardhi yao bila fidia au kwa fidia kidogo huweza kusababisha amani ya nchi kuyumba au kupotea.

Alitolea mfano wa Kaya 86 ziliondolewa kupisha mgodi wa dhahabu wa Geita katika kijiji cha Mtakuja na watu zaidi ya 250 hawana pakuishi kwa takribani miaka miwili sasa.

Aidha alisema wananchi wa kijiji cha Namawala Kilombero wako hatarini kuondolewa kijijini kupisha mwekezaji asiyejulikana zaidi ya asilimia 62 ya ardhi yao yenye ukubwa wa kilomita za mraba 9272.54 zinachukuliwa na kuathiri zaidi ya wakazi 10,000 na watoto wa skuli zaidi ya 2000.

Naye Prosista Paul, alisema hakuna nchi yoyote duniani ambayo imeendelea bila uwekezaji na kwamba jitihada za kugeuza maliasili za nchi kuwa katika rasilimali kwa kutumia nyenzo kama mtaji, teknolojia na nguvu kazi jambo litakalomaliza migogoro mingi ya ardhi hapa nchini.

Alisema tafiti mbali mbali zinaonyesha uwekezaji hufanywa na kundi dogo huku zaidi ya asilimia 70 ya wakazi wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara hujishughulisha na kilimo kwa ajili ya kujikimu na siyo kilimo cha uwekezaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.