Habari za Punde

Waziri Mbarouk Akutana na Balozi Mdogo wa Oman


Na Abdi Shamnah

SERIKALI ya Oman imesema iko tayari kutekeleza makubaliano yote yaliofikiwa kati ya nchi hiyo na Zanzibar katika nyanja mbali mbali, zikiwemo za habari, utamaduni,utalii na michezo, kama hatua ya kuendeleza uhusiano uliopo kati ya nchi mbili hizo.

Hayo yameelezwa na Balozi mdogo wa Oman aliopo Zanzibar, Mansour Al Busaid, wakati alipokuwa na mazungumzo na Waziri wa Habari,Utamaduni,Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk ofisini kwake Mnazi Mmoja.


Viongozi hao walipata nafasi ya kuzipitia kumbu kumbu za makubaliano ‘memorundum of understanding’ ziliosainiwa Augost, 17,2010 baina ya iliokuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar na Wizara ya Urithi na Utamaduni ya Oman, pamoja na kuangalia maeneo mengine ambapo zinaweza kushirikiana.

Balozi Mansour alisema kuna mambo mengi ya kushirikiana katika nyanja za sanaa na utamaduni kupitia katika maonyesho mbali mbali pamoja na ile ya kubadilishana vitabu vitakavyoonyesha maingiliano yaliokuwepo kati ay watu wa nchi hizi.

Alisema Oman inakususdia kuangalia ni aina gani ya vifaa vilivyo mashuhuri ambavyo vilipata kutumika hapo zamani na sasa vimepotea katika makumbusho ili kuvileta nchini na kusaidia katika juhudi za kukuza utalii.

 Alishauri kuwepo utaratibu wa kushirikiana na kubadilishana uzoefu kwa wasanii (wanamuziki) wa Zanzibar ili wapate  fursa ya kwenda Oman sambamba na wale wa Oman kuja nchini.

Balozi huyo alimhakikishia Waziri Mbarouk kuwa nchi yake ina wataalamu wazuri katika masuala ya uhifadhi wa nyaraka, hvyo iko tayari kuisaidia Zanzibar ili kuona nyaraka zote muhimu zinatunzwa kwa faida ya baadae.

Mapema Waziri Mbarouk alimweleza Balozi huyo kuwa  Zanzibar imedhamiria kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu na wenzao wa Oman,  na kuiomba nchi hiyo kuangalia uwezekano wa kusaidia matengenezo katika majengo ya Makumbusho ambayo yako katika hali mbaya, huku baadhi ya nyaraka zikiwa zimeshaharibika.

Aidha aliiomba Oman kusaidia matengenezo ya magofu mbali mbali ili kulinda historia zake , kutoa nafasi za masomo kwa Wazanzibari pamoja na kupata fursa ya kujifunza jinsi nchi hiyo ilivyopata maendeleo makubwa ya kiutalii bila kuathiri utamaduni wake.

Vile vile aliiomba nchi hiyo kusaidia upatikanaji wa mafunzo kwa mafundi wa Shirika la Utangazaji (ZBC –TV) sambamba na haja yakubadilishana vipindi kati ya kituo hicho cha Televisheni na ile ya Taifa nchini Oman.

Nae Mkurugenzi wa Makumbusho na Mambo ya Kale, Dk. Amina Ameir, alitilia shime matengenzo ya majengo ya Beit el Ajaib, Kasri la Mfalme pamoja na Kaburi na kuelezea umuhimu mkubwa wa kuyanusuru kabla uharaibifu haijawa mkubwa zaidi.

Pia aliiomba nchi hiyo kusaidia juhudi za Idara yake za kuanzisha kitengo cha Marine Achiology Unit, kwa kukipatia vifaa vya kutendea kazi pamoja na taaluma kwa wafanyakazi wake.

Dk. Amina aliomba kupatiwa fursa za mafunzo kwa wafanyakazi wa Idara hiyo, ili kufanikisha malengo ya  kufungua makumbusho zaidi katika Mikoa ya Unguja na Pemba, na kuweka bayana uhaba wa wafanyakazi wenye taaluma ya kutosha unaoikabili Idara yake.  

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Ali Saleh Mwinyikai, alisema mambo yaliokubaliwa katika ‘Memorundum’ hiyo ni makubwa sana lakini bado ukubwa wake haujaonekana na kushauri kuteremshwa katika ngazi za watendaji kwa utekelezaji kutoka ngazi za Mawaziri ilipo sasa. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.